15 wafariki ajali ya basi Tanzania. Picha: Getty

Basi hilo la abiria lililohusika kwenye ajali, lilikuwa likitoka Newala kwenda Dar es Salaam.

Breki ya basi hilo inadaiwa kufeli na kusababisha vifo vya abiria papo hapo na hata kusababisha maafa ya wapita njia.

"Ajali hiyo ilitokea Jumapili saa moja asubuhi na kusababisha vifo vya watu 12 papo hapo kwenye basi walilokuwa wakisafiri pamoja na wapita njia wawili waliokuwa karibu na eneo la tukio," alisema Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, ACP John Makuri.

ACP Makuri ameongeza kuwa zaidi ya majeruhi 30 wamekimbizwa hadi hospitali ya rufaa ya Nyango kupokea matibabu.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma rambirambi zake kwa wale wote waliofariki kwenye ajali hiyo na kutuma pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Aidha, rais Samia amewaagiza wahusika wa usalama kuimarisha doria na usalama barabarani kupitia ukaguzi dhabiti haswa wakati huu ambapo watu wengi wanapoelekea kuadhimisha msimu wa likizo ya mwisho wa mwaka.

Nawapa pole wafiwa waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ya basi iliyotokea eneo la Mtama mkoani Lindi na kusababisha vifo vya watu 15. Mwenyezi Mungu awe faraja kwetu sote, awarehemu ndugu zetu hawa waliotutoka na kuwajalia majeruhi pona ya haraka. Tunapoelekea msimu wa mwisho wa mwaka, naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama barabarani kuongeza usimamizi wa sheria na ukaguzi.

Rais Samia Suluhu Hassan

Mapema mwaka huu, watu ishirini walifariki baada ya basi lililokuwa likisafiri kati ya Shinyanga na Dar Es Salaam kugongana na lori Nzega, mkoani Tabora, na kutajwa kuwa ajali mbaya zaidi mkoani Tabora mwaka huu.

TRT Afrika na mashirika ya habari