Shirika la Afya Duniani (WHO) linaamini kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Mpox kwenye baadhi ya nchi za Afrika utadhibitiwa ndani ya miezi sita ijayo.
Kauli hiyo inakuja wakati shehena ya kwanza ya chanjo ya ugonjwa huo ikitarajiwa kuwasili nchini Congo, taifa lililoathirika kwa kiasi kikubwa na idadi ya maambukizi.
“Kupitia uongozi bora na ushirikiano dhabiti kati ya wadau, tunaamini kuwa tunaweza kudhibiti ugonjwa ndani ya miezi sita ijayo,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema siku ya Ijumaa.
Bara la Afrika limepokea kiwango kidogo cha chanjo kukabiliana na ugonjwa huo unaoendelea kusambaa maeneo tofauti.
Kiwango cha chini cha vifo
Licha ya ongezeko la maambukizi mapya, bado dunia inashuhudia kiwango cha chini cha vifo.
WHO imeutangaza ugonjwa huo barani Afrika kama hali ya dharura kiulimwengu, ikitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka.
Kirusi kipya cha ugonjwa huo kimegundulika katika nchi mbalimbali zikiwemo Congo, Rwanda na Kenya.
Ugonjwa wa Mpox huambukizwa kwa njia ya kugusana na dalili zake ni pamoja na homa, kichwa kuuma na vipele.
Njia ya kuzuia
WHO inakadiria kuwa karibu chanjo 230,000 zitatumwa Kongo na nchi zingine zilizoathiriwa.
Shirika hilo pia linalenga katika kuongeza uelewa kuhusu hatua za kuzuia.
Licha ya hali ya usambazaji wa chanjo kuwa ni mdogo, WHO inasema inafanya kazi kuharakisha ufikiaji kwa nchi zinazohitaji.
Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kuelewa jinsi mpox inavyoenea barani Afrika ili kutumia vyema chanjo zinazopatikana.