Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India huku akiendelea na ziara yake nchini India.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru Profesa Santishree Dhulipudi Pandit alimpa rais Samia shahada hiyo ya heshima wakati wa hafla maalum ya kumtunuku iliyoandaliwa mjini New Delhi nchini India leo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa India Dk. S. Jaishankar amesema kuwa ni jambo la fahari kubwa kwa taifa la India kumtunuku heshima ya Udaktari Rais Samia Suluhu Hassan katika Chuo kikuu cha Jawaharlal Nehru.
"Kwa kumheshimu na kumtunuku shahada hii ya kielimu, sio tu tunatambua ushirika wake wa muda mrefu na India lakini pia inaashiria kipengele hiki maalum ya uhusiano baina ya nchi zetu", Waziri wa Mambo ya Nje wa India Dk. S. Jaishankar amesema.
"Ninatoa tuzo hii maalum (shahada ya heshima ya causa) kwa mtoto wa kike wa Kitanzania anayeishi katika maeneo ya mbali zaidi nchini. Nataka wajue kuwa kwa bidii na kujitolea, dari zote za glasi zinaweza kubomolewa", Rais Samia aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.