Wizara ya Afya ya nchini Tanzania imetuma timu ya wataalamu mkoani Kagera kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa Marburg katika eneo hilo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Jenista Mhagama, wataalamu hao watachukua sampuli na kufanya vipimo vya maabara.
Hata hivyo, waziri huyo amesisitiza kuwa, hadi kufikia Januari 15 2025, hapakuwa na taarifa zozote wa wahisiwa wa ugonjwa huo, kama ilivyoripotiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Wizara inapenda kuwahakikishia wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani, kuwa Tanzania imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na itaendelea kutoa taarifa zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za WHO, ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu, ugonjwa huu ulishawahi kuripotiwa katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.
Ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate , mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa.