Ronald Sonyo
TRT Afrika, Dodoma, Tanzania
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameziagiza mamlaka zinazohusika na usafirishaji nchini humo kuhakikisha hadi ifikapo mwezi Julai, mwaka huu kuwa safari za reli ya mwendo kasi zinaaza rasmi kati ya Dar es Salaam na mji mkuu wa Dodoma.
Rais Samia amesema wananchi wamechoshwa kusikia kila siku safari zinaahirishwa.
Awali, Novemba, 2022, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilisema kuwa linatarajia kuanza rasmi kwa safari za reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ya kilomita 300 kati ya Dar es Salaam na Morogoro kuanzia Februari mwaka jana.
Hata hivyo, ahadi hiyo haikutimia. Baadae mwishoni mwa 2023, katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Uchukuzi nchini Tanzania Profesa Makame Mbarawa, alisema matarajio ya kuanza kwa awamu hiyo ya kwanza ni mwishoni mwa Januari mwaka 2024.
"Ni jambo la kufurahisha ambalo nafikiri Watanzania wengi watalifurahia. Mwisho wa mwezi unaokuja, yani mwezi wa Januari, tutaanza rasmi kutumia usafiri wetu wa SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, kwa ajili ya abiria, sio mizigo," alisema Prof. Mbarawa.
Rais Samia amebainisha kuwa vipande vya reli hiyo vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora zimefikia zaidi ya asilimia 90.
"Nimekuwa nikisia mabadiliko ya tarehe ya kuanza kwa safari za treni kupitia Reli ya Mwendo Kasi-SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kwa kweli wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Na sasa nielekeze, ifikapo mwisho wa mwezi Julai, 2024 safari ya Reli ya SGR kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma ziwe zimeanza," alisema Mkuu huyo wa nchi.
Amesema Serikali imepata udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Afrika utakaowezesha uendelezaji wa kipande cha Tabora- kigoma na uvinza Msongati.
Tarehe 30, mwezi Disemba, mwaka jana, Shirika la Reli katika taarifa yake kwa umma, lilisema tayari limepokea vichwa vitatu vya treni za umeme na mabehewa 27 ya abiria.
"Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania ilifanya manunuzi ya vichwa 17 na mabehewa mapya 59 ya abiria kwa ajili ya uendeshaji wa reli ya kiwango cha kimataifa-SGR. Mpaka sasa, Shirika limepokea vichwa vya treni ya umeme vinne (4) kati ya 17 kutoka kampuni ya Hyundai Rotem na mabehewa 56 kati ya 59 kutoka kampuni ya 'Sung Shin Rolling Stock Technology' (SSRST) ya nchini Korea Kusini," ilisema taarifa hiyo.
Katika salamu zake za mwaka mpya kwa Taifa ambayo imejikita zaidi katika mapito ya mwaka ulioisha wa 2023, pia amekiri kuwepo kwa changamoto kadhaa za upatikanikaji wa umeme lakini akaahidi kuwa Serikali inalifanyia kazi jambo hilo.
"Nimekuwa nikisia mabadiliko ya tarehe ya kuanza kwa safari za treni kupitia Reli ya Mwendo Kasi-SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kwa kweli wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Na sasa nielekeze, ifikapo mwisho wa mwezi Julai, 2024 safari ya Reli ya SGR kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma ziwe zimeanza."
Hotuba yake ya dakika 35 na sekunde 17 ambayo iliangazia mafanikio ya mwaka huu na kutoa mwelekeo wa mwaka ujao. Pia aliitumia nafasi hiyo, kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Licha ya kuwa hajaorodhesha mageuzi yaliofanyika lakini amesema mwaka uliokwisha wa 2023 ulikuwa wa mageuzi, huku akisema 2024 utakuwa wa utekelezaji zaidi.
Kukamilika kwa mradi wa Reli ya Mwendo Kasi, kunasubiriwa kwa hamu, baadhi ya wachumi wakisema, mradi huo utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa umma.
Mnamo mwaka 2017, Kenya ilikuwa ni taifa pekee katika nchi za Afrika Mashariki, kuzindua rasmi safari za treni ya mwendo kasi kutoka pwani ya nchi hiyo Mombasa hadi mji mkuu Nairobi. Kama ilivyo kwa Tanzania, lengo la mradi huu, ni kuziunganisha nchi nyengine za Afrika Mashariki kama Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Ethiopia. Hata hivyo, inaweza kuchukua miaka kadhaa kabla ya ndoto hiyo kutimia.