Jumla ya mashirika 7 nchini Tanzania yamesababisha hasara ya bilioni 400 (Dola Milioni 155), Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa nchi hiyo amesema.
Akikabidhi ripoti yake ya mwaka 2022/23 kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Machi 28 mjini Dodoma, Mkaguzi Mkuu wa nchi hiyo, Charles Kicheere amebainisha kuwa Shirika la Ndege la Nchi hiyo (ATCL), ni kati ya taasisi zilizopata hasara kubwa katika uendeshaji wake.
Kulingana na ripoti hiyo, hasara ya Shirika hilo imekuwa kwa asilimia 61, na kufikia shilingi bilioni 57 (Dola Milioni 22) kutoka bilioni 35.2 (Dola Milioni 13.5), katika miaka iliyopita.
Hasara ya Shirika hilo inakuja siku chache baada ya Serikali ya Tanzania kununua ndege mpya, aina ya Boeing 737- Max 9.
"Hasara hiyo imeongezeka wakati ATCL imepokea bilioni 31.55 kusaidia uendeshaji wake," amesema Kicheere.
Hata hivyo, ripoti hiyo pia imeanisha baadhi ya mashirika yaliyoweza kufanya vizuri katika kupunguza hasara zake kwa taifa.
Taasisi hizo ni pamoja na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mashirika mengine ambayo yameendelea kuisababishia hasara serikali ya Tanzania ni pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ya TANOIL.
Agosti mwaka jana, Rais Samia aliyataka mashirika na taasisi za serikali kujiendesha kibiashara ili kuwafanya Watanzania kununua hisa na kuyaongezea ufanisi.
Tanzania ina jumla ya taasisi 248 zinazosimamiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina.