Rais Samia ameimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu / Picha : AFP

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kubuniwa afisi ya naibu wa Waziri Mkuu pamoja na kuunda wizara mpya, ikiwa ni wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi zilizotawanywa kutoka kwa iliyokuwa wizara moja ya ujenzi na uchukuzi.

Hii ni katika mabadiliko madogo yaliyofanywa na mama Samia katika baraza la mawaziri na makatibu wakuu.

Mh. Dkt. Doto Mashaka Biteko, atachukua wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu ambapo atajukumiwa kusimamia uratibu wa shughuli za serikali. Vile vile Dkt. Mashaka atahudumu kama Waziri wa Nishati.

Mh. January Yusuf Makamba, amehamishwa kutoka wizara ya Nishati na kupewa wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Mh. Stergomena Lawrence Tax amehamishwa kutoka wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenda kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mh. Innocent Lugha Bashungwa atakuwa Waziri wa Ujenzi na kuhamishwa kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mh. Prof Makame Mnyaa Mbarawa, amehamishwa kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi.

Mh. Anthony Peter Mavunde ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini, na kuhamishwa kutoka Wizara ya Kilimo alikohudumu kama Naibu Waziri.

Mh. Jerry William Silaa, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makaazi.

''Katika mabadiliko hayo, Rais Samia ameimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu watakaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.'' Kama ilivyosema taarifa kwa vyombo vya habari.

Kijumla Rais Samia amewateua, Naibu Waziri mkuu, Mawaziri wanne (4), Naibu Mawaziri watano (5), Makatibu Wakuu watatu (3), Naibu Makatibu Wakuu watatu (3), na wengine wamehamishwa kutoka wizara moja hadi nyingine.

TRT Afrika