Kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya 'simu janja', kulingana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)./Picha: Getty

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanisha ongezeko la matumizi ya 'simu janja', miongoni mwa watumiaji wa huduma za simu nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti ya robo mwaka, iliyotolewa Oktoba 20, 2024 na mamlaka hiyo, asilimia ya simu janja nchini humo hadi kufikia asilimia 33.85 kutoka asilimia 31.55 iliyorekodiwa mwezi Juni 2024.

Kulingana na TCRA, nchi hiyo imeshuhudia uwepo wa simu janja zipatazo 22,029,561, ambayo ni sawa na asilimia ya 33.85 ya ueneaji wa vifaa hivyo.

Aidha, ripoti hiyo pia inaonesha ongezeko la simu za rununu kutoka asilimia 82.6 hadi asilimia 84.83.

Kulingana na TCRA, mkoa wa Rukwa unaongoza ukiwa na majaribio 5,571, ikifuatiwa na Morogoro iliyo na majaribio 5,486 wakati mkoa wa Dar es Salaam unashika nafasi ya nne, ukiwa na vitendo 959 vya ulaghai.

Ripoti hiyo pia inaonesha upungufu wa majaribio ya ulaghai kwa asilimia 28./Picha: Wengine

"Mikoa ya Rukwa na Morogoro ndiyo inayoongoza, ikiwa na zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai nchini. Mbeya, Dar es Salaam na Arusha zinafuata kwa majaribio ya ulaghai kwa zaidi ya asilima moja hadi 10," inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Mikoa mingine ya Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Kusini Pemba ina idadi ndogo ya majaribio, huku kila mkoa ukirekodi asilimia 0.01, ripoti hiyo inaonesha.

Aidha, jumla ya idadi ya vikoa vilivyosajiliwa iliongezeka kutoka 30,698 mwishoni mwa Juni 2024 hadi 31,584 mwishoni mwa Septemba 2024.

Jumla ya idadi ya vikoa vilivyosajiliwa nchini Tanzania./Picha: TCRA

Kwa mujibu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, usajili wa kikoa co.tz, uliongezeka kutoka 24,085 mwezi Juni 2024 hadi kufikia 24,796 mwezi wa Septemba.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo, imetoa takwimu za mawasiliano ya simu, pesa mtandao, Intaneti, utangazaji, posta na usafirishaji wa vifurushi na vipeto, na huduma nyingine zinazohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Takwimu zimeandaliwa kulingana na viwango vya Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) vya kukusanya na kuandaa takwimu za huduma za mawasiliano/TEHAMA.

TRT Afrika