Uhalifu wa kimtandao bado unaendelea kushika kasi kwenye sekta ya mawasiliao nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), matukio ya ulaghai katika huduma za mitandao yamefikia 21,788 katika kipindi cha kati ya Oktoba hadi Disemba mwaka 2023.
Mwaka 2022, TCRA iliripoti vitendo 12,603 katika kipindi kama hicho.
Kulingana na mdhibiti huyo wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania, mkoa wa Rukwa ndio unashika nafasi ya kwanza kwa vitendo vya namna hiyo ikiwa na matukio 7,666, huku mtandao wa Tigo ukiwa kinara wa kupitisha jumbe za kilaghai.
Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba visiwani Zanzibar, ndiyo yenye matukio machache zaidi ya kilaghai, kulingana na TCRA, ikiwa na matukio 6 na 5 mtawalia.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dr Jabir Bakari kufungiwa kwa laini zisizosajiliwa kutasaidia, kwa kiasi kikubwa, kupunguza matukio ya utapeli na ulaghai mitandaoni.
Mwanzoni mwa 2023, mamlaka hiyo ilitangaza azma ya kuzifungia laini milioni mbili zisizohakikiwa.
Hata hivyo, ripoti ya TCRA inaonesha kuwa jumla ya laini za simu 30,309 zimefutiwa matumizi katika robo ya nne ya mwaka 2023, ukilinganisha 34,848 zilizofungwa katika robo ya tatu.
Wakati huo huo, ripoti hiyo inaonesha ongezeko la matumizi ya huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu.
Kulingana na TCRA, huduma hizo zimeongezeka kutoka 526,245,314 mwezi Oktoba, hadi kufikia 549,529,470 kwa mwezi Disema mwaka 2023.