Ummy Mwalimu

Idadi ya watu waliowekwa karantini wilayani Bukoba, Mkoa wa Kagera nchini Tanzania, imeongezeka kutoka 193 hadi 205 kutokana na maelezo ya Wizara ya Afya.

Waziri Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa wataalamu wa afya wameendelea kufuatilia watu wote ambao walichangamana na wagonjwa wa Marburg na kuwaweka karantini kwa muda wa siku 21 ili kubaini iwapo wana kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Waziri huyo aliwataka wakazi wa Mkoa wa Kagera kuendelea na shughuli zao za kila siku na kutoogopa ugonjwa huo na kuwataka kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono, kwa kutumia vitakasa mikono, na kutoshikana mikono, pamoja na kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Alisema kuwa wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii wapatao 1322 wameajiriwa kwa muda wa miezi mitatu mkoani Kagera kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu katika ngazi ya jamii kwenye kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Marburg.

Aidha Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dk Issesanda Kaniki amesema kwa kushirikiana na manispaa ya Bukoba na wadau wengine wataendelea kuweka mitambo ya kunawia mikono katika maeneo ya kituo kikuu cha mabasi na soko kuu.

Pia, katika barabara ya kuelekea Geita, Mwanza, Kahama, Dar es Salaam na mikoa mingine, kutawekwa kituo maeneo ya Kemondo ili abiria wote wapimwe joto lao kando ya barabara ya Karagwe, Mtukula, pia katika eneo la Kyaka Misenyi, kitawekwa kituo cha kupima abiria wote wanaotoka katika barabara hiyo.

Waziri Ummy atatembelea kata ya Maruku na Kayangereko, walikopatikana watu walioambukizwa ugonjwa wa Marburg, eneo ambalo watu 205 wamewekwa karantini, na kituo cha matibabu kwa wagonjwa wa Marburg badae wiki hii.

TRT Afrika