Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Serikali ya Tanzania imeazimia kuliomba Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kibali cha kukarabati baadhi ya miundombinu ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti, inayopatikana kaskazini mwa nchi hiyo.
Msemaji Mkuu wa nchi hiyo, Mobhare Matinyi amewaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania imeomba ridhaa kutoka UNESCO kutengeneza barabara zake muhimu kwa kutumia tabaka gumu ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kupunguza adha ya kufanya matengenezo kila baada ya msimu wa mvua kuisha.
"Kutokana na uharibifu wa barabara uliosababishwa na mvua za El Nino serikali imefikia maamuzi ya kuomba kibali hicho ili kuimarisha miundombinu yake isiharibiwe tena na mvua," amesema Matinyi wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Uamuzi huo ni kutokana na kuwa hifadhi ya taifa ya Serengeti ni sehemu ya urithi wa dunia, ambayo iliingizwa kwenye orodha hiyo na UNESCO mwaka 1981.
Kulingana na Matinyi, mvua kubwa zilizonyesha Oktoba 2023, zimefanya baadhi ya barabara ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutopitika kirahisi, na hivyo kuilazimu Serikali ya Tanzania kuja na hatua za muda mrefu ambazo hazitoathiri uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori.
"Kwa sasa, tunalenga kuboresha barabara kuu nne ndani ya hifadhi hii kwa kuweka tabaka gumu, na hivyo kurahisisha usafiri kwa watalii na watumiaji wengine wa barabara hizo," amesema.
Kulingana na Matinyi, barabara hizo zinaunganisha mikoa ya Arusha, Simiyu, Manyara, Mara na Shinyanga kupitia hifadhini humo wenye mtandao wa kilomita 291.
Hifadhi ya Serengeti inafahamika sana kwa tukio la uhamaji wa Nyumbu milioni 1.5 kila mwaka, na ndio hifadhi bora zaidi barani Afrika, kwa mara ya 5 mfululizo.