Meta, kupitia mtandao wake wa Facebook utaanza kuwalipa watengeneza maudhui wenye wafuasi 5,000 na kuendelea./Picha: Getty

Watengeneza maudhui katika mtandao wa Facebook nchini Tanzania, wataanza kuvuna mapato yao ya mitandaoni kupitia jukwaa kwa la Meta.

Kwa mujibu wa Meta, watengeneza maudhui wenye wafuasi 5,000 na kuendelea, kwenye mtandao wa Facebook ndio watakuwa wamekidhi vigezo hivyo vya malipo.

Kwa mujibu wa meneja wa sera wa Meta katika ukanda wa Afrika Mashariki, Desmond Mushi malipo hayo yataanza kufanyika ndani ya wiki tatu zijazo.

Hata hivyo, ili malipo hayo yafanyike watengeneza maudhui hayo wanapaswa kufikia vigezo mbalimbali, vikiwemo idadi ya matangazo ambayo jukwaa la Meta litaweka katika maudhui yao, usajili wa wafuasi, na 'nyota' katika kurasa zao.

"Kama kila kitu kitaenda sawa, malipo hayo yataanza kufanyika ndani ya wiki mbili hadi tatu zijazo," aliongeza.

Mbali na Facebook, watengeneza maudhui kwenye mtandao wa Instagram nao wataanza kupokea mapato ya kazi zao, baada ya wiki sita.

TRT Afrika