Chama cha Mapinduzi (CCM) cha nchini Tanzania kimetoa salamu za pole kwa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kufuatia kifo cha mjumbe wake wa, Ally Mohamed Kibao.
Mwili wa Kibao ulipatikana katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali na kwenda kuhifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mwananyamala, kabla haujatambuliwa na ndugu zake, wakiwemo pia viongozi wa CHADEMA, waliokuwa wanaongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe, siku ya Septemba 8, 2024.
Mwanachama huyo wa CHADEMA aliripotiwa 'kutekwa' na watu wasiojulikana akiwa ndani ya basi siku ya Septemba 6.
"Nimeona kwenye Vyombo vya Habari kuanzia asubuhi mpaka sasa nitoe pole kwa Chama cha CHADEMA kwa kumpoteza mmoja wa Wajumbe wa Sektarieti bwana Ali Kibao nimekuwa nikifuatilia sisi ni vyama vya siasa linapokuja suala la ubinadamu Chama unaweka pembeni, nawapa pole kwa msiba", alisema Katibu wa NEC-Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.
Chama hicho, pia kimelitaka Jeshi la Polisi nchini Tanzania litimize wajibu la kuendelea na uchunguzi wa jambo hilo.
Mapema Septemba 6, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, alitangaza tukio la kutekwa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya chama hicho, Ally Mohamed Kibao.
Kulingana na Mnyika, tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 6, 2024, eneo la Kibo, karibu na Tegeta, wakati Kibao akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga kwa basi la Tashrif.