Katika miaka ya hivi karibuni ukame umeathiri mamilioni ya watu Afrika Picha : Oxfam

"Niger ni nchi katika eneo la Sahel, sehemu kubwa ya eneo hilo imeathiriwa na ukame, hasa katika maeneo ya vijijini. Hata katika baadhi ya maeneo ya mijini, kuna mifuko ya ukame," Sani Ayouba anaelezea TRT Afrika.

Kijana huyu ni mkuu wa shirika la vijana Young Volunteers for the Environment (JVE-Niger), linalopigania utunzaji wa mazingira.

Jukumu lake linampeleka kila siku kuona athari za ukame kwa maisha ya watu nchini Niger, haswa wanawake.

"Hasa katika maeneo ya vijijini ambako asilimia 70 ya watu wanaishi, wanawake wanategemea kabisa shughuli za kilimo na ufugaji. Uhaba wa mvua, ukame na hali ya jangwa vina athari katika shughuli hizi. Hii inazidisha ukosefu wa usawa na umaskini," anasema.

Mboga iliyoathirika

"Hawawezi kuzalisha vya kutosha kulisha familia zao na kuuza katika masoko ya vijijini ili kukidhi mahitaji ya kila siku ya watoto," anaongeza Sani Ayouba.

Kuenea kwa jangwa ni jambo la asili linalorejelea uharibifu unaoendelea wa udongo katika maeneo kame, nusu kame na yenye unyevunyevu.

Kwa kiasi kikubwa husababishwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu, huzidisha kuzorota kwa mimea, mmomonyoko wa udongo na kusababisha uhamiaji wa watu.

Ukame umesababisha uhaba mkubwa katika maeneo mengi ya Afrika Picha : Oxfam

Kuenea kwa jangwa na ukame huathiri kilimo cha bustani, aina ya kilimo ambacho wanawake wa Niger wanajishughulisha nacho.

Upatikanaji wa maji ni mgumu kwa sababu kutokana na ukame, visima vya bustani vya sokoni hukauka. Kutokana na hali hiyo, mazao ya kabichi, nyanya au hata maboga ambayo wanawake hao huzalisha, kwa ajili ya kutumia na kuuza hayakidhi matarajio yao.

Wanyama pia huathirika kwa sababu nyasi huwa chache kutokana na uhaba wa mvua.

Benki za chakula

"Hii ndiyo sababu Niger inatekeleza mradi unaojulikana kama ZARESE wa kuboresha usalama wa chakula na kukuza mipango ya wakulima katika maeneo yenye hatari kubwa ya mazingira na kijamii" anafafanua Bibi Issa Hamsatou Kailou, mshauri wa kiufundi katika mawasiliano na mahusiano ya umma wa Baraza la Taifa la Mazingira kwa maendeleo endelevu.

Mradi huu unalenga kuchangia katika kurejesha mifumo ya uzalishaji ili kuboresha maisha ya watu katika jamii zilizo hatarini kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uhamiaji.

Inajumuisha uchimbaji wa visima vya ufugaji, visima vya bustani ya soko, juenzi wa kinga za mito , uanzishwaji wa hifadhi za chakula cha mifugo na ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa.

Niger ni miongoni mwa nchi za Sahel zinazopoteza mititu yake kwa kasi  Picha : Reuters 

Kwa hivyo ZARESE inakusudia kuongeza na kusambaza uzalishaji endelevu wa kilimo-mseto na wafugaji, kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na kuwapa walengwa fursa ya kupata ardhi ili kukuza maendeleo shirikishi ya ndani ambayo yanastahimili mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo unalenga zaidi wakulima vijana, wanawake na familia za wahamiaji zinazoongozwa na wanawake.

Kulinda mfumo wa ikolojia

Mwaka huu, kaulimbiu ya Siku ya Dunia ya Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame iliyoadhimishwa Juni 17 ni ''Ardhi yake. Haki zake.''

Kwa kuchagua mada, Umoja wa Mataifa ''unasisitiza kwamba kuwekeza katika upatikanaji sawa wa ardhi kwa wanawake na mali zinazohusiana ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maisha yao ya baadaye na mustakabali wa uhai.''

Siku ya Dunia ya Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame inaadhimishwa kuambatana na azimio la Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa mwaka 1994.

Kusudi lake ni kuongeza ufahamu wa sababu na hatari za matukio haya na kuhimiza juhudi katika kiwango cha kimataifa ili kuepusha athari mbaya kwa wanadamu na mifumo ya ikolojia ya sayari.

TRT Afrika