Taasisi isiyo ya kiserikali nchini Benin yapambania haki za wanawake

Taasisi isiyo ya kiserikali nchini Benin yapambania haki za wanawake

Mwanaharakati wa nchini Benin ashawishi jamii za nchi hizo kuwapa wanawake haki za kumiliki ardhi.
Wanaume wengi katika nchi za Afrika wana haki ya kumuliki ardhi./Picha: Tamou Charaf Yarou  

Na Firmain Eric Mbadinga

Madame Zouléath, hakuwahi kudhani kuwa ipo siku atamiliki ardhi, kijijini kwao Niaro.

Mabadiliko hayo yalitokana na majadiliano kati ya mumewe na mwanzilishi wa Tonkouro, shirika lisilo la kiserikali lenye kuangazia haki za wanawake kwenye kumiliki mali.

Akiwa anamiliki hekta 2.5 za ardhi kwa jina lake, Zouléath anahisi amewezeshwa kwa kila njia. Anategemea kuandaa shamba ambalo atapanda viazi ambavyo vitaisaidia kupata kipato.

Zouléath, ambaye kijiji chake kiko kaskazini mwa idara ya Borgou nchini Benin, inaweza kuwa ubaguzi katika ukanda wa mashambani licha ya ulinzi wa kikatiba na kisheria kwa wanawake kupata mali kwa kuzaliwa na kuolewa.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na harakati za kuwapa wanawake umiliki wa ardhi. Picha:Tamou Charaf Yarou

Katiba ya Benin ya mwaka 1990 inatoa hakikisho kwenye usawa wa kijinsia ambao pia huenda kwenye upatikanaji wa ardhi.

Kulingana na utafiti wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), chini ya asilimia 30 ya wanawake nchini Benini wanamiliki ardhi.

Katika nchi nyingi za Kiafrika, wanaume ndio wenye kumiliki ardhi japokuwa kazi nyingi za kilimo hufanywa na wanawake.

Uhalisia huu unaupa Umoja wa Afrika wasiwasi na umeahidi kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030, angalau asilimia 30 ya ardhi katika bara zima iwe chini ya umiliki wa wanawake.

Nchini Benin, mashirika mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakiwasaidia wanawake wanaokumbana na upinzani wa kitamaduni na kimila.

Kupambana na upendeleo

Mwanzilishi wa Tonkouro, Tamou Charaf Yarou anaamini kwamba sheria inaweza kutekelezwa iwapo tu mambo ya kijamii yaliyokita mizizi yatabadilishwa.

"Wanawake hukumbana na vikwazo vikubwa vinavyowazuia kuongeza uzalishaji wao. Hizi ni pamoja na upatikanaji wa ardhi na usalama. Suala la upatikanaji wa rasilimali za ardhi kwa wanawake sio tu la kisheria lakini pia la kijamii, kitamaduni na kisiasa," anaiambia TRT Afrika.

Akiwa ni muumini mkubwa wa majadiliano, Yarou alianza dhamira ya kuhamasisha watu kwa kuwasiliana na watu katika miji na vijiji, mwaka 2019.

Tonkouro ilianza kuonesha mabadiliko mwaka huu, licha ya kuwa na rasilimali chache.

"Siku moja, niliwauliza wanakijiji wenzangu watatu kutoka Niaro katika wilaya ya Sinendé kwa nini walikuwa wanakataa kuwaruhusu wake zao kumiliki ardhi na kupanda mimea," Yarou anasimulia.

Kampeni za uhamasishaji zinaendelea kuendeshwa ili kukuza umiliki wa ardhi kwa wanawake. Picha: Tamou Charaf Yarou

“Waliniambia wakifanya hivyo jamii haitawaheshimu, nikawauliza nini kitatokea baada ya kufa, kimya kilitanda chumbani, msimu uliofuata kila mmoja akawapa wake zao shamba. Naweza kusema ilisaidia sana."

Mwanasosholojia kutoka Benin Edith Assangbé angependa kuona serikali inainua lengo lake la umiliki wa ardhi wa wanawake na kuimarisha masharti ya kisheria.

"Ni kweli sheria ipo. Hata hivyo, katika maeneo ya vijijini, ushawishi wa kitamaduni unaweza kuzuia baadhi ya wanawake kuchukua ardhi. Wengi wa wanawake hawa pia hawajui haki zao za ardhi," anaiambia TRT Afrika.

Hali hii inaangazia umuhimu wa kampeni za uhamasishaji kama zile zinazoendeshwa na Yarou.

Vipaumbele vinavyofanana

Kulingana na takwimu za Benki ya Dunia, kilimo kinachangia asilimia 25 ya pato la taifa barani Afrika. Hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba wanawake ndio nusu ya ya wafanyakazi.

Kwa kuzingatia mienendo ya uchumi wa kilimo, upatikanaji mkubwa wa umiliki wa ardhi kwa wanawake unaweza kuchangia katika pato la Taifa la nchi nyingi za Afrika.

Taasisi hiyo ya Yarou inalenga kutoa mafunzo kwa wanawake katika ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika shughuli za kuzalisha kipato kama vile ufinyanzi na utengenezaji wa siagi na shughuli nyinginezo.

"Kwa kuwawezesha wanawake wa vijijini, tunaweza kubadilisha elimu kwa ujumla. Kwa kupata ardhi, wanawake hawa wanaweza kuanza kilimo, kupata fedha za kujitegemea, kulisha familia zao, kupeleka watoto wao shule, kusaidia kukabiliana na uhaba wa chakula, na kusaidia wanawake wa vijijini," Yarou anaongeza .

Kando na tafiti hizo kutoka taasisi kama vile Oxfam, wakala wa Ubelgiji Enabel, UNICEF na CARE International, Yarou hufanya uchunguzi wake mwenyewe ili kuandaa mpango kazi wake.

"Taasisi ya Tonkouro, yenye maana ya 'mwanamke' katika lugha yangu ya asili ya Bariba, ni kielelezo cha lengo langu la kuwawezesha wanawake," anasema.

Yarou, ambaye amekuwa akifanya kazi za jumuiya kwa miaka mitano, anatumia ujuzi wake wa jiografia kutafuta fedha kwa ajili ya misheni ya Tonkouro. Kwa muda mfupi, uanachama wa taasisi umeongezeka hadi kufikia wafanyakazi 17 waliojitolea na wengi wa kujitolea.

TRT Afrika