Na Hamisi Iddi Hamisi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Istanbul ni jiji maarufu duniani ikiwa ni eneo pekee linalopatikana katika mabara mawili, la Asia na Ulaya.
Umaarufu wake ulimfanya Napoléon Bonaparte, aliyekuwa kiongozi wa himaya ya Kifaransa ya wakati huo kutamka kwa kinywa chake mwenyewe na kusema: Laiti ‘Dunia ingekuwa ni nchi, basi Istanbul ungekuwa mji mkuu’!
Hata kabla kuitwa Istanbul, jiji hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 5,461 limewahi kujulikana kama Constantinople.
Miaka 571 imepita sasa tangu jeshi la dola ya Ottoman likiongozwa na Sultan Mehmed wa pili kufanya kile ambacho hakikufanywa na kamanda au jeshi lingine la Kiislamu katika karne nyingi.
Sio tu kwamba Waturuki waliudhibiti “Malkia wa Miji,” lakini pia walifuta kwa ufanisi mabaki ya mwisho ya utawala wa Roma ya Mashariki. Utawala uliojulikana pia kama Byzantine na kukomesha moja ya falme kubwa zilizowahi kushuhudiwa ulimwenguni.
Ushindi huo ulifungua njia ya kukua kwa Dola ya Ottoman na kuenea kwa Uislamu katika maeneo ya Balkan.
Wanahistoria wengi wanalichukulia tukio hili kama alama ya mwisho wa enzi za kati na mwanzo wa kipindi cha mapema cha Ulaya ya kisasa.
Sultan Mehmed II ni nani?
Akiwa na umri wa miaka 21 tu, kuanzia kukomesha utawala wa Roma ya Mashariki na kuikomboa Istanbul hadi kupanua Utawala wa Ottoman kwa zaidi ya kilomita za mraba milioni 2.2, Sultan Mehmed II aliacha alama isiyoweza kufutika kwenye historia.
Sultan Mehmed II alipata jina la Mehmed Mfunguzi (Fatih) baada ya kuikomboa Istanbul.
Alizaliwa Machi 30, mwaka 1432, huko Edirne. Sultan Mehmed II alifundishwa na akili bora za wakati wake. Ingawa alisoma Qur’an na kupata ujuzi wa kina wa Uislamu, alifunzwa pia mawazo ya Magharibi na alizungumza lugha kadhaa kama vile Kiajemi, Kiarabu, Kigiriki cha kale na Kitaliano.
Alikuwa Sultan wa Dola mara mbili, mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 12 tu baada ya baba yake Sultan Murad II kujiuzulu.
Lakini baada ya miaka miwili Sultan Murad alirudi na kuchukua kiti chake mpaka alipofariki.
Wakati huo Sultan Mehmed II alikuwa amehamia mji wa Manisa na alifunga ndoa huko. Miaka miwili baadaye yaani mwaka 1448, Mehmed II alijiunga na baba yake katika vita vya Kosovo, ambapo alipata ufahamu wa masuala ya kijeshi.
Baada ya baba yake kufariki mwaka 1451, Sultan Mehmed II alichukua kiti cha enzi kama kiongozi mwenye uzoefu na sifa zaidi kuliko alivyokuwa wakati wa utawala wake wa kwanza.
Kulingana na wanahistoria mashuhuri wa Uturuki, maktaba ya Sultan Mehmed II ilisheheni vitabu kuhusu Jiometri, Dini, Uhandisi, Unajimu, Hisabati, Akiolojia, Jiografia na Falsafa.
Aliwalinda wasomi wa dini zote na asili zote na akawaruhusu kuchapisha kazi zao kuhusu mambo ya kisayansi.
Kufunguliwa kwa Istanbul mwaka 1453
Sultan Mehmed II alikuwa jasiri pale alipoamua kuiteka Istanbul baada ya kukusanya kati ya askari 100,000 hadi 200,000.
Mpango wake ulikuwa ni kuuzingira mji huu kutoka baharini na nchi kavu.
Sultan Mehmed II aliamuru hatua ambayo haikutarajiwa, ambayo iliingia katika historia kama ujanja wa kijeshi wenye akili na wa kutisha.
Aliwaagiza askari wake kubeba meli za kivita nchi kavu kwa kuziviringisha juu ya magogo katika eneo la Galata, lililoko upande wa Ulaya, ili kupata nguvu kubwa.
Kazi haikuwa rahisi kwani jeshi la Ottoman liljikuta uso kwa uso na kuta za himaya ya mpinzani za mji wa Istanbul zisizoweza kupenyeka.
Mizinga ilipigwa kuelekea kuta hizo ngumu na mwingine kutua kwenye kuta hizi bila kusababisha athari yoyote ile.
Wakati wa awamu ya mwisho ya operesheni ya kijeshi ya siku 50, handaki la chini ya ardhi lilichimbwa ili kuweka vipuli vya mlipuko mkubwa chini ya ukuta. Mlipuko huo, pamoja na upigaji wa mizinga, ulivunja sehemu ya ukuta, na kutengeneza mwanya kwa wanajeshi wa Ottoman kuingia ndani ya mji wa Istanbul.
Mnamo Mei 29 mwaka 1453, jiji la Istanbul lilianguka, na utawala wa karne nyingi wa Dola ya Byzantine ukamalizika. Sultan Mehmed II akaitwa Mehmed Mkombozi, na Dola ya Ottoman ikawa kituo kikuu cha nguvu duniani.
Sultan Mehmed II alifariki Mei 3, 1481 akiwa na miaka 49 akiwa pia ameshiriki katika safari 25 za kijeshi na kuifanya Istanbul kuwa mji mkuu wa himaya yake.