Kenya na Somalia zimekubaliana kufungua tena mipaka yao  / Photo: AFP

Kenya na Somalia zimekubaliana kuimarisha mawasiliano na habari za mipakani huku zikiamua kufungua tena vituo vyao vya mpaka.

"Tunaangalia uwezekano wa kufungua tena mpaka na tumeamua kwamba mpaka kati ya Somalia na Kenya utafunguliwa tena kwa awamu kwa muda wa siku 90 zijazo," waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Kithure Kindiki aliambia vyombo vya habari.

Kenya iliamua kufunga baadhi ya maeneo ya mpaka wake na Somalia mwezi Oktoba 2011 kwa sababu za kiusalama. Nairobi ilisema ni kutokana na wimbi la ugaidi linalofanywa na Al-shabaab, kundi linalo chukuliwa kuwa la kigaidi na nchi zote mbili.

"Tumeweza kupitia upya mipangilio iliyowekwa ili kurahisisha watu wetu kutembea kwa uhuru zaidi, kwa kuangalia upya taratibu za viza ili kuhakikisha kadiri inavyowezekana tunarejesha harakati za watu huru," Kindiki aliongeza. .

Ufunguzi upya wa mipaka utafanyika kwa awamu.

Ndani ya siku 30 kuanzia tarehe 15 Mei 2023, mpaka wa Mandera-Bulahawa utafunguliwa tena.

Ndani ya siku 60, kituo cha mpaka cha Liboi-Harhar kitafunguliwa tena, na ndani ya siku 90, eneo la Daresalam katika mpaka wa Kiunga-Ras Kamboni litafunguliwa tena.

Katika taarifa ya pamoja nchi hizo mbili zinasema kwamba zinakubali kuna changamoto ya mipaka zikiwemo itikadi kali za kidini, uhalifu, uhamiaji haramu , ugaidia na masuala mengine ya kiusalama.

"Kufungua mipaka kunawanufaisha watu wa nchi hizo mbili na hii inaambatana sana na wazo la makubaliano ya mikataba ya shirika letu la Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD ambayo inainua ushirikiano wa wanachama wetu " Nuur Mohamud Sheekh, msemaji wa katibu mtendaji wa IGAD ameiambia TRT Afrika.

"Pia ni katika mwelekeo mwema wa kuinua mfumo wa eneo la biashara huria la Bara la Afrika, ambalo linalenga kukuza biashara ya ndani ya Afrika." Mohamud anaongeza.

Nchi hizo mbili sio tu washirika wa kibiashara lakini pia zinahusiana kwa utamaduni, huku watu wa asili ya Kisomali wakiwa raia nchini Kenya.

TRT Afrika