Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud anasema serikali yake inajitahidi katika kuleta utulivu kwa maeneo ambayo yaliokolewa kutoka kwa Al Shabaab.
Al-Shabaab ni kikundi cha kigaidi ambacho Umoja wa Mataifa unakielezea kama "tishio kubwa kwa amani na usalama".
"Tunategemea Umoja wa Mataifa kuongeza uwekezaji muhimu katika maeneo hayo yaliyookolewa , watu hawa kama raia wetu wamenyimwa huduma za kiraia kwa muda mrefu, " Rais Mohamud alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Guterres yuko nchini Somalia kwa ziara rasmi.
Rais Mohamud pia ameiomba Umoja wa Mataifa kuondoa kabisa vikwazo vya silaha. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda wa vikwazo hivyo hadi Novemba 15, 2023, likitaja tishio la kuendelea la kundi la kigaidi la Al-Shabaab kwa amani na utulivu wa eneo hilo.
Vikwazo hivyo vimeanza tangu mwaka 1992 kwa nia ya kuzuia utiririshaji wa silaha nchini humo baada ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Vikwazo vilipunguzwa hapo awali, hiyo ilisaidia sana, na tunatarajia vitolewe kabisa katika siku za usoni ," alisema rais Mohamud.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametilia mkazo ombi la kimataifa kwa Somalia.
"Pia niko hapa kutoa tahadhari kuhusu mahitaji ya msaada mkubwa wa kimataifa, kwa sababu ya shida za kibinadamu zinazokabili Somalia," alisema Gutteres, "msaada mkubwa wa kibinadamu kuhusiana na ujenzi usalama wa Somalia na msaada mkubwa wa kibinadamu katika kuleta utulivu na maendeleo. ya nchi.”