Hamisi Iddi Hamisi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Simba itakuwa itakuwa inaombea miujiza ya mwaka 2003 kujirudia, pale itakaporusha karata yake ya mwisho dhidi ya Al Ahly ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo.
Mchezo huo wa wa pili katika hatua ya robo fainali, unapigwa leo usiku kwenye dimba la Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, nchini Misri.
Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania, Al Ahly waliibuka washindi kufuatia bao la mapema zaidi lililowekwa kimiani na Ahmed Nabil Kouka.
'Wekundu hao wa Misri', wanahitaji suluhu au ushindi wa aina yoyote ile, ili kutinga hatua ya nusu fainali.
Kwa upande wao, Simba Sports Club, maarufu kama 'Wekundu wa Msimbazi watakuwa wanaombea miujiza ya mwaka 2003 itokee, ili wawe katika nafasi nzuri ya kuingia hatua ya nusu fainali.
Ikumbukwe kuwa, Simba, iliyokuwa ikifundishwa na Mkenya James Aggrey Siang'a iliwatoa Zamalek, tena nchini kwao, kwa mikwaju ya penati, kufuatia uhodari golikipa Juma Kaseja.
Kwa upande wao, Yanga, ambao ni watani wa jadi wa Simba, watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya wajukuu wa mzee Madiba, Mamelodi Sundowns katika mchezo utakopigwa kwenye uwanja wa Loftus Versfeld jijini Johannesburg, Afrika Kusini saa 3 usiku.
Mbali na kuwa mchezo wa Simba dhidi ya Al Ahly ndio unatarajiwa kutazamwa zaidi kutokana na ukubwa wa timu hizo, wingi wa mashabiki na ushawishi wao katika soka, lakini mchezo wa Yanga dhidi ya Mamelodi unatazamiwa kuwa wa kuvutia na kuburudisha hasa ikizingatiwa matokeo yao ya awali ya sare ya bila kufungana.
Kutoshana nguvu katika mchezo wao awali inaweza kuwa sababu kuu ya kuwapa watazamaji wa mtanange wa leo ladha adimu na murua kwani kila timu itakuwa ikitafuta ushindi kwa hali na mali, na hivyo kuwajibika kuonesha kandanda safi, katika muda wote wa mchezo.
Historia kuandikwa tena na Tanzania
Iwapo Simba na Yanga zitafanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali, basi Tanzania itakuwa imeandika historia, kwa mara nyingine tena.
Ikumbukwe kuwa, Tanzania iliweka historia kwa kutoa timu mbili kwenye hatua ya robo fainali hapo awali, katika mashindano hayo makubwa kwenye ngazi ya vilabu barani Afrika.