Hili ni tukio linalovutia mamilioni ya watazamaji kutoka kila pande ya dunia./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kila mwaka, eneo la Kogatende, linalopatikana kwenye kingo za mto mara ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania, hufurika maelfu ya watu, wakiwa na shauku ya kuona tukio moja tu.

Hili ni tukio lenye kuvutia mamilioni ya watazamaji, kutoka kila pembe ya dunia; tukio la uhamaji wa kundi la nyumbu, kutoka hifadhi ya taifa ya Serengeti kuelekea pori la akiba la Masai Mara nchini Kenya, na kisha kurejea tena Tanzania.

Katika hifadhi ya taifa ya Serengeti, zaidi ya Nyumbu milioni 1.3, pundamilia 200,000, swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000, kila mwaka, husafiri umbali mrefu kwenda kutafuta malisho na maji.

Safari hiyo huanzia hifadhi ya taifa ya Serengeti hadi Masai Mara nchini Kenya, kabla ya msafara huo kurejea tena nchini Tanzania.

Mzunguko huo ni endelevu. Kulingana na wataalamu wa ikolojia ya eneo la Serengeti, Nyumbu na wanyama wengine, huzunguka katika ikolojia hiyo kwa zaidi ya kilomita 1,000 kila mwaka, na kuufanya mzunguko huo kuwa wa kipekee kabisa duniani.

Hata hivyo, chanzo cha moja ya maajabu haya ya asili duniani, ni eneo la Ndutu lenye kilomita za mraba zaidi ya 8,000, na linajumuisha sehemu ya kreta ya Ngorongoro, Olduvai Gorge ambayo ni chimbuko la historia ya zamadamu, na sehemu ya hifadhi ya Serengeti.

“Ni tukio kubwa sana duniani linatokea katika hifadhi ya taifa ya Serengeti,” Catherine Mbena, Afisa Uhifadhi Mwandamizi anayeshughulikia Mawasiliano katika Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(TANAPA).

Safari ya wanyama hao huanzia kati ya mwezi wa pili na wa tatu kila mwaka na hutanguliwa na hatua ya kuzaliwa kwa nyumbu katika eneo la Ndutu.

Kulingana na Mbena, Nyumbu wana uwezo wa kuahirisha zoezi la kuzaa, kwa sababu za kiusalama wa watoto wao na uhakika wa chakula na maji.

Muhifadhi huyo anasema kuwa Nyumbu wengi huamua kuzalia katika eneo la Ndutu kutokana na uhakika wa maji na chakula unaopatikana hapo.

“Majani ya eneo hilo yana madini ya kutosha yenye Phosphorous, Calcium na Magnesium na ndio maana Nyumbu akidondosha tu mtoto, haichukui muda mrefu kabla hajaanza kutembea mwenyewe,” anailezea TRTAfrika.

Kila mwaka, eneo la Kogatende, linalopatikana kwenye kingo za mto mara ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania, hufurika maelfu ya watu, wakiwa na shauku ya kuona tukio hilo./Picha: Wengine

Kinachoimarisha misuli ya miguu ya nyumbu hao wadogo ni maziwa yanayotokana na majani yenye virutubisho hivyo, anasema Mbena. Mara tu baada ya kuzaliwa, safari ya uhamaji wa nyumbu hao ndio inaanza, kutafuta malisho na maji.

Baada ya Ndutu, eneo lililopo Tanzania, msafara huo huelekea eneo la kati la Seronera kwenda Kilawira na hatimaye Kogatende, wakijiandaa kuvuka mto Mara.

Idadi ya nyumbu wavukao mto huo, kulingana na wahifadhi ni milioni 1.5, kila mwaka.

“Wakati maeneo mengi ya upande ya Serengeti yanakuwa makavu kuanzia mwezi wa nane, hali ni tofauti kwa upande wa pili, ambapo mvua nyingi zinashuhudiwa,” Mbena anaelezea.

Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa eneo la Masai Mara, ni asilimia 25 mpaka 30 ya Nyumbu wanaobakia Kenya, katika msafara huo.

Hata wakivuka mto, bado wanakuwa wanarandaranda maeneo ya Serengeti, na hukaa upande wa pili kati ya miezi miwili hadi mitatu kabla ya kurudi upande wa Tanzania, mwezi Septemba.

Athari za Tabia Nchi

Kwakuwa nyumbu wanafuata maji na mvua ndio kivutio chao, mzunguko mzima unaweza kubadilika kutokana na kuwahi au kuchelewa kwa mvua.

Mbena anasema kuwa utaratibu mzima huvurugika, kwani Nyumbu hao huhairisha zoezi la kuhama.

“Hata hivyo, mwisho wa lazima waende, kwani ndio sehemu maisha yao,” anasema.

Hali kama hiyo imewahi kushuhudiwa mwaka 2022 baada ya mvua kuchelewa kunyesha, upande wa Kenya.

Mchango wa kivutio hiki kwa Utalii

Kulingana na TANAPA, tukio hili huvutia watalii wengi sana ndani ya hifadhi ya Serengeti na kuitangaza nchi ya Tanzania.

Afisa Uhifadhi Mwandamizi huyo anaweka wazi kuwa kwa siku eneo hilo hushuhudia zaidi ya magari 800 ya watalii, wanaokuja kustaajabia tukio hilo.

“Hesabu hii ni kutoka geti la Nabi tu, bado hatujazungumzia njia zingine,” anasema Mbena.

Bugudha kutoka wa waongoza Utalii

Mara nyingi, shauku ya kushuhudia tukio hili hugeuka kuwa bugudha na kero kwa wanyama hawa.

Kulingana na Mbena TANAPA wamejitahidi mara kwa mara kukutana na waongoza utalii na kujadiliana namna ya kuondoa kero na bugudha wakati wa zoezi la uvukaji mto Mara.

“Ukweli ni kwamba, wanyama hawa wanaweza wakaghairi kuvuka ikiwa kuna kelele nyingi za watalii na mingurumo ya gari,” anailezea TRTAfrika.

Adha ya Msafara

Wakati wote wa msafara wao, Nyumbu hukutana na wanyama wakali kama vile Simba, Chui na Fisi na hivyo hushambuliwa na kuuwawa.

Changamoto kama hiyo, pia hujitokeza wakati wa kuvuka maji yaendayo kasi ya Mto Mara, kwani baadhi hushambuliwa na mamba, viboko wakati wengine huchukuliwa na maji.

Serengeti imeibuka kama hifadhi bora kabisa Afrika kwa mara ya tano mfululizo.

Moja ya vivutio vinavyolifanya eneo hilo kuwa la kipekee, ni tukio la uhamaji wa Nyumbu.

TRT Afrika