Mabingwa hao wa Sudan wana mlima mkali wa kupanda baada ya kufungwa 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Kigali, Rwanda.

Vigogo wa soka nchini Sudani, Al-Merreikh watawasili Dar es Salaam tarehe Septemba 27, 2023 majira ya saa tisa alasiri kwa saa za Afrika ya Mashariki kwa Shirika la ndege la Rwanda, Rwandair.

Al- Merreikh watawakabili mabingwa wa soka nchini Tanzania Yanga katika mechi itakayoamua timu ipi inafuzu kucheza hatua ya makundi hapo Septemba 30,2023 katika uwanja wa Chamazi , uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, mabingwa hao wa Sudan wana mlima mkali wa kupanda baada ya kufungwa 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Kigali, Rwanda.

Hivyo, wanahitaji ushindi wa 3-0 au zaidi ili kusonga mbele.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema.

"Kimsingi sisi hatuna rekodi nzuri kucheza hatua ya makundi,"

"Hilo halina siasa, ni uhalisia,"

"Lakini kwa wakati huu tuna imani kubwa tutavunja huo mwiko,"

"Dhamira yetu ni kubwa mno kuanzia kwa wachezaji mpaka kwa mashabiki," amesema Kamwe na kuongeza.

"Tumesikia kauli za Kocha wa Al-Merrikh anasema kuwa Young Africans inaogopeka Afrika,"

"Sisi tumesoma Cuba, tunamwelewa, hawezi kutuchota,"

"Tutauchukulia mchezo wetu wa pili kwa umakini mkubwa,"

"Amesema pia anakuja kufunguka hapa, kwetu sisi ni taarifa njema kwa sababu mnara haukusoma Rwanda, hivyo tukipishana nao itakuwa fursa ya kusimamisha mnara", amesema.

Joto la mechi hiyo linazidi kupamba na matumaini ya Yanga ni kusonga mbele. Lakini kocha wa Al- Merreikh Osama Nabieh anasema wamejipanga kuhakikisha wanapindua matokeo ya Rwanda. Je, nini utabiri wako msomaji wa TRT Afrika kuelekea mechi hii?

TRT Afrika