Wanakijiji waliuwa simba sita kusini mwa Kenya  / Photo: AP

Simba sita waliuawa Ijumaa, kufuatia madai ya uvamizi katika kijiji cha Nashipa katika kaunti ndogo ya Kajiado kusini mwa Kenya.

Ripoti zilionyesha kuwa simba 11, akiwemo mmoja mtoto walitangatanga katika kijiji hicho cha Nashipa , Ijumaa usiku kutoka hifadhi ya kitaifa ya Amboseli, kutafuta chakula.

“Simba hao waliua mbuzi kumi na mmoja na mbwa mmoja usiku wa ijumaa. Kwa bahati mbaya, hili si tukio la pekee kwani katika wiki iliyopita, Simba wengine wanne wameuawa na kusababisha jumla ya simba kumi kuuawa katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli,” ilisoma sehemu ya taarifa ya huduma ya wanyamapori nchini Kenya yaani Kenya Wildlife Service.

Inaripotiwa simba hao walishambulia nyumba moja na kuua kondoo 11 na mbwa katika kile ambacho wakazi walielezea kuwa usiku wa hofu.

Jumamosi asubuhi, wanakijiji waliokuwa wamejihami kwa mikuki waliwasaka simba hao na kuwaua sita kati yao. Mizoga mingi ilikuwa na mishale na mikuki.

Shirika la ulinzi wa Wanyama ulimwenguni, yaani World Animal Protection, imekashifu mauaji ya simba sita kutoka mbuga ya kitaifa ya Amboseli, nchini Kenya

“Ingawa tunaelewa na kuhurumia hasara iliyosababishwa na jamii, tunalaani vikali kitendo cha kikatili cha kuua simba bila kuzingatia mbinu mbadala za kutatua migogoro,” taarifa ya shirika la World Animal Protection, limesema katika taarifa.