Shirika la Taifa la ndege la Kenya, Kenya Airways limetangaza kuondoa marufuku ya miaka mitatu ya safari zake za ndege kuelekea Mogadishu, Somalia.
Kampuni hiyo ilifichua mipango ya kurejesha safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Mogadishu, na safari ya kwanza ya ndege imepangwa kufanyika Februari 14, 2024.
Hatua hiyo, "inalingana na kuongezeka kwa biashara na kuongezeka kwa usafiri wa anga kati ya Kenya na Somalia," Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja wa Kenya Airways Julius Thairu alisema Jumatano.
Habari hizi zinakuja wiki moja tu baada ya Somalia kuweka historia ya kuwa mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Novemba 24 katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Arusha, Tanzania.
Kurahisisha usafiri
Kukubalika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mwanachama wa nane kunakuja baada ya kusubiri kwa muda wa miaka 11 tangu Somalia ilipowasilisha ombi lake.
Kurejeshwa kwa usafiri wa anga sio tu kunakuza mafungamano lakini pia kunafungua fursa za biashara na utalii kati ya mataifa hayo mawili.
Kulingana na Shirika hilo la Ndege, safari za ndege za moja kwa moja zinatarajiwa kurahisisha utaratibu wa usafiri, kutoa njia rahisi na bora ya usafiri kwa abiria na mizigo sawa.
Katika miaka ya hivi karibuni, mvutano kati ya Kenya na Somalia umekuwa mkubwa kutokana na sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na mzozo wa mipaka ya bahari, madai ya kuingilia masuala ya ndani ya Somalia na hali ya usalama nchini Somalia.