Rais wa Kenya William Ruto Jumatatu alishutumu Wakfu wa Ford wenye makao yake Marekani kwa kufadhili "machafuko" na kufadhili maandamano ya kuipinga serikali ambayo yaliingia katika ghasia mbaya mwezi uliopita.
Taifa hilo lenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki limetumbukia katika machafuko ya kisiasa kutokana na maandamano hayo, ambayo yalianza kama mikutano ya amani iliyoongozwa na Gen-Z wa Kenya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi lakini yameingia katika kampeni kubwa dhidi ya Ruto na utawala wake.
Makumi ya watu wameuawa tangu maandamano hayo yaanze mwezi mmoja uliopita, ikiwa ni siku mbaya zaidi mnamo Juni 25 wakati umati wa watu wenye hasira kali ulipovamia bunge na polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji.
"Wale wanaofadhili machafuko katika Jamhuri ya Kenya, aibu kwao kwa sababu wanafadhili ghasia dhidi ya taifa letu la kidemokrasia," Ruto alisema katika hafla moja katika mji wa Rift Valley, Nakuru.
"Nataka kuwauliza watu wa Ford Foundation, hizo pesa wanazotoa kufadhili vurugu, watafaidika vipi," Ruto aliambia umati mkubwa uliokusanyika kumsikiliza akizungumza.
"Tunaenda kuwaambia kama hawapendi demokrasia nchini Kenya, kama wanaenda kufadhili vurugu nchini Kenya, kama watafadhili machafuko, tutawataja kwa majina na tutawaambia kwamba wajirekebishe au wanaondoka."
Ofisi ya Ford Foundation ya Afrika Mashariki mjini Nairobi na ubalozi wa Marekani haukujibu mara moja maombi ya maoni.
Shirika hilo, lililoanzishwa mwaka wa 1936 na Edsel Ford, mwana wa mwanzilishi wa Ford Motor Company Henry Ford, linafanya kazi kote ulimwenguni na linalenga kuendeleza haki ya kijamii na kukuza maadili ya kidemokrasia.
Ruzuku
wakfu huo umetoa ruzuku kwa makundi mbalimbali ya haki za Kenya na mashirika ya kiraia kwa miongo michache iliyopita.
Ruto, ambaye anang’ang’ania kuficha mzozo mbaya zaidi wa urais wake wa karibu miaka miwili, awali ameshtumu viongozi wa kigeni ambao hawakutajwa majina kwa kuchochea machafuko wakati wa maandamano.
Maandamano ya mitaani yamepungua hivi majuzi, lakini wanaharakati wametaka maandamano mapya kufanyika Jumanne.