Mahakama Kuu ya Kenya imekataa kubatilisha amri ya awali iliyositisha utekelezaji wa mswada wa fedha wa 2023.
Kesi iliwasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah na Wakili Otiende Omollo.
Walidai kuwa baadhi ya vipengele katika mswada huo ambao ulikuwa unafaa kuanza kutimizwa Julai 1, vinatishia haki ya kumiliki mali, na kukiuka katiba kwa ujumla.
Serikali ya rais William Ruto iliunga mkono sheria hiyo ikidai kuwa mabadiliko yanahitajika ili nchi ipate fedha zaidi kutoka ndani , na ipunguze kukopa nje.
Kwa hivyo sheria hii ilipendekeza ongezeko ya ushuru katika sekta tofauti.
Jaji Mugure Thande ametupilia mbali ombi la serikali iliyotaka kubatilishwa agizo alilokuwa ametoa la kuzuia kutekelezwa sheria hiyo.
Amesema serikali haikutoa sababu za kutosha kumtaka aondoe amri hiyo.
Waziri wa fedha aliambia mahakama kwamba serikali ilikuwa inapoteza zaidi ya dola milioni nne kila siku kwa kukosa kukusanya kodi tangu maagizo ya kusimamisha utimizaji sheria hiyo kutolewa mnamo Juni 30.