Serikali ya Kenya imemuomba balozi wa Marekani nchini humo Meg Whitman kutotilia maaniani maneno ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga nakuendelea na shughuli zake za kiserikali pamoja na maafisa halali wa serikali.
Makamu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ameyataja maneno ya Raila Odinga kuwa kelele za mtu asiyekubali kushindwa baada ya Odinga kumtishia kushinikiza kuondolewa kwa balozi huyo wa Marekani kwa 'kuunga mkono matokeo ya uchaguzi ya 2022.
"Ninataka kumwomba Balozi Meg kupuuza kelele na kuzoea njia ya Wakenya ya kufanya mambo -Malalamiko ya kudumu mwaka baada ya mwaka, anapaswa kuwa makini na kuendelea na kazi yake," Gachagua alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano juu ya ugatuzi uliofanyika jijini Eldoret Magharibi mwa nchi.
Balozi Whitman alijikuta katikati ya malumbano ya Odinga na serikali ya Ruto huku amejikuta kati kati ya wimbi la malumbano kufuatia matamshi yake ya kusifia uchaguzi mkpuu wa Kenya wa 2022.
Gachagua pia alimpa onyo Raila Odinga kutozungumzia hadharani maneno asiyokuwa na mamlaka nayo akimtaja kama 'raia wa kawaida.'
"Huwezi kuzungumza katika jukwaa la umma, mbele ya televisheni ya taifa, na kusema kwamba una uwezo wa kumrudisha balozi wa Marekani aliyeidhinishwa kwa nchi hii na serikali ya Marekani. Wewe ni Mkenya wa kawaida tu na huna mamlaka kama hayo,” aliongeza.
Makamu wa rais Gachagua alisema kuwa Balozi Whitman amefanya vikao vya mashauriano na rais pamoja na viongozi wa wizara mbali mbali na ameridhishwa na namna uendeshaji wa nchi ulivyo, na hata kupanua mahusiano y akibiashara kati ya Marekani na Kenya.
Rais Odinga amekuwa akilalamikia matokeo ya uchaguzi ya 2022 akidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda kihalali japo kesi yake ya kupinga matokeo ilitupiliwa mbali na mahakama kwa kukosa ushahidi.
Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya William Ruto, Raila na viongozi wengine wa upinzani wamekuwa wakizua kila aina ya malalamishi dhidi ya serikali, punde zaidi ikiwa kulalamikia gharama ya maisha iliyotokana na mfumko wa bei na ongezeko la kodiu wanazotozwa wananchi pamoja na kuwekwa kodi mpya ya nyumba.
Mashauriano yameanza kati ya viongozi wa Upinzani na ujumbe wa serikali kutatua hili kufuatia maandamano yaliyoongozwa na upinzani yanayolaumiwa kusababisha hasara kubwa kiuchumi pamoja na uharibifu wa mali za umma na vifo kadhaa.