Muungano wa Wafanyakazi wa Sekta ya Usafiri wa Anga nchini Kenya umesema Jumatatu kwamba wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Kenya na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya watagoma kuanzia Agosti 19.
Hii ni kutokana na pendekezo la uwekezaji kutoka kwa kampuni ya India, Adani Airport Holdings, katika uwanja mkuu wa ndege nchini humo.
Mgomo huo unaweza kusababisha usumbufu mkubwa kwa Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways, na kwa shughuli za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, kitovu muhimu cha usafiri barani Afrika.
"Tutafikiria upya nia yetu ya kushiriki katika hatua za kiviwanda...ikiwa tu mkataba wa Adani Airport Holdings Limited utatelekezwa kwa ukamilifu," alisema Moss Ndiema, Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga nchini Kenya.
Mwezi uliopita, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya ilisema pendekezo la uwekezaji kutoka kwa Kampuni ya Adani Airport Holdings ni pamoja na njia ya pili ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Uwekezaji wa Adani Holdings
Kampuni ya Adani Holdings kutoka India ya Adani Group, kupitia kampuni yake tanzu ya Adani Airport Holdings Limited, ilionesha nia ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Tayari, wawekezaji hao wametenga kiasi cha dola bilioni 1.85 kupanua sehemu ya uwanja wa ndege wa Kimaitaifa wa Jomo Kenyatta.
Iwapo mchakato huo utaidhinishwa, basi kampuni hiyo kutoka India itakuwa imejihakikishia kukusanya asilimia 18 ya mapato yake ya kila mwaka, ndani ya miaka 30, tangu kuanza kwa uwekezaji huo.
Kampuni hiyo pia imelenga kubadilisha muonekano wa JKIA, ikiwa ni pamoja na kujenga sehemu ya pili ya kurukia ndege ndani ya uwanja huo wa kimataifa nchini Kenya.
Mchanganuo zaidi unaonesha kuwa kampuni ya Adani itatumia dola milioni 750 kujenga jengo la abiria, sehemu ya maegesho ya ndege na sehemu za kutokea.
Mradi huo, unategemewa kukamilika mwaka 2029.