Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imeamua kutuma Jopo la Wazee wa SADC kufanya mazungumzo na Serikali ya Msumbiji na viongozi wakuu wa upinzani kuhusu mazingira ya utata baada ya uchaguzi nchini Msumbiji.
Jopo hili linafaa kutoa ripoti kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC ifikapo tarehe Januari 15, 2025.
Huu ulikuwa ni uamuzi wa Mkutano wa wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Januari 5, 2025 na kujadili Hali ya Kisiasa na Usalama baada ya Uchaguzi wa Msumbiji.
Kikao hicho kiliongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na Nancy Gladys Tembo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, aliyemuwakilisha Mwenyekiti anayekuja wa kitengo cha ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Rais Lazarus McCarthy Chakwera wa Malawi.
Tangu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2024 kumekuwa na ghasia nchini Msumbiji baada ya upinzani kukataa matokeo ya uchaguzi ambao ulimpa ushindi Daniel Chapo wa chama tawala cha FRELIMO dhidi ya mpinzani wake Venancio Mondlane.
Baraza la Katiba lilisema Mondlane alipata asilimia 24 ya kura za urais ikilinganishwa na 65% ya mgombea urais wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo.
Venancio Mondlane wa upinzani amekuwa akipinga ushindi huo.
Chapo, 47, anatazamiwa kuapishwa Januari 15, 2025 akichukua nafasi ya Rais Filipe Nyusi mwishoni mwa ukomo wake wa mihula miwili.
SADC yatafuta suluhu
Mkutano wa SADC ulibainisha kuwa na wasiwasi kuhusu kuzorota kwa hali ya kisiasa na usalama baada ya uchaguzi Msumbiji, ikiwa ni pamoja na athari za kijamii na kiuchumi nchini humo na athari mbaya kwenye minyororo ya ugavi wa bidhaa muhimu.
Rais Samia alisisitiza kuwa kanda ya SADC haiwezi kupuuza kile kinachotokea katika nchi ya Msumbiji, hasa inapoathiri moja kwa moja mfumo wa kijamii na kiuchumi wa kanda nzima ya SADC.
Rais Hichilema wa Zambia alisisitiza kwamba hali ya kisiasa na usalama nchini Msumbiji haiathiri tu watu wa Msumbiji lakini pia inazuia biashara ya kikanda katika sekta muhimu kama vile nishati na usafiri.
Alisisitiza haja ya Jumuiya ya SADC kuunga mkono kwa dhati jitihada za kurejesha amani na utulivu nchini Msumbiji kupitia hatua za pamoja katika kukuza usalama na ushirikiano wa kikanda.
Mkutano huo uliagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya nchi mbalimbali kupendekeza hatua za kulinda njia za biashara za kikanda, njia za kibinadamu, na usambazaji wa nishati wakati wa kutafuta suluhisho kwa changamoto za kisiasa na usalama katika Msumbiji.