Rais Filipe Nyusi: "Lazima sote tuungane karibu na komredi Daniel Francisco Chapo" / Picha: Reuters

Chama tawala cha Frelimo nchini Msumbiji, kimemtangaza Daniel Francisco Chapo kuwa mgombea urais wa chama hicho kupishana na rais aliye madarakani Filipe Nyusi.

Ingawa ni mtu asiyejulikana katika siasa za kitaifa, Chapo ni gavana wa Inhambane, mkoa wa kusini mwa Msumbiji.

Chapo, ambaye ni mtangazaji wa zamani wa redio, alizaliwa 1977, na uteuzi huu umemfanya kuwa mgombea wa kwanza wa chama tawala FRELIMO aliyezaliwa baada ya uhuru wa nchi hiyo.

Uamuzi huo uliafikiwa baada ya kupata kura 225 (takriban asilimia 94% ya kura) kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na kamati kuu ya chama, taarifa ya chama ilisema.

FRELIMO imekuwa ikitawala nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu ilipojipa uhuru mnamo 1975 na inatumai Chapo ataizolea chama hicho ushindi mwingine kwenye uchaguzi ujao wa Oktoba 9.

"Lazima sote tuungane karibu na komredi Daniel Francisco Chapo, katika safari ya kutaka ushindi wa uchaguzi Oktoba ijayo," Nyusi alisema.

Licha ya katiba ya Msumbiji kuruhusu tu mihula miwili ya miaka mitano, uvumi ulienea awali kwa vyombo vya habari kwamba rais Nyusi angesaka muhula wa tatu baada ya kuchaguliwa tena kama kiongozi wa chama mnamo 2022.

Kielimu, Chapo ana shahada ya sheria na shahada ya Uzamili katika usimamizi wa maendeleo na amewahi kushikilia majukumu ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwa msimamizi wa wilaya za Nacala na Palma.

Reuters