Kumetokea hitilafu katika upatikanaji wa huduma ya Intaneti katika mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki Mei 12, 2024, shirika la uchunguzi wa mtandao la Netblocks limesema na kuongeza kuwa tukio hilo lilihusishwa na kushindwa kufanya kazi kwa mifumo ya SEACOM na EASSy inayopatikana chini ya bahari.
Tanzania na kisiwa cha Ufaransa cha Mayotte ndizo zilizopata athari kubwa, wakati Msumbiji na Malawi zilishuhudia athari ya wastani, ilisema Netblocks, kupitia ukurasa wake wa X.
Kampuni ya mtandao ya Cloudflare ilisema kwenye moja ya akaunti zake za X kuwa inafuatilia mwenendo kuwa kukatika kwa intaneti kunaendelea nchini Tanzania, Malawi, Msumbiji na Madagascar kutokana na hitilafu zilizoripotiwa kwenye EASSy na nyaya za SEACOM.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Nape Nnauye, amekiri kutokea kwa tatizo hilo lililosababisha kukosekana kwa huduma za intaneti pamoja na huduma za simu za kimataifa.
"Jitihada za kutatua tatizo hilo zinaendelea. Aidha, wakati utatuzi wa tatizo hilo unaendelea, upatikanaji wa huduma za intaneti pamoja na huduma za simu za kimataifa utakuwa wa kiwango cha chini kwa kutumia njia mbadala mpaka tatizo husika litakapotatuliwa," aliandika Waziri huyo kwenye ukurasa wake wa X.