Machi 2019 kimbunga kilichoitwa "IDAI" kiliua watu 1,593 na kuathiri wengine zaidi ya milioni 3 katika nchi za Msumbiji, Malawi, Madagascar na Zimbabwe. / Picha: AP

Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Kimbunga ni dhoruba kali ya hali inayokuwa na upepo wenye nguvu pamoja na mvua nyingi na inaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na hata kuwauwa watu.

Mei 2024 watabiri wa hali ya hewa walionya kuwa kimbunga kitaikumba Kenya na Tanzania. Kimbunga hiki kikaitwa "Hidaya."

Wavuvi wa Tanzania wakisafiri kwa boti yao katika Bahari ya Hindi wakijiandaa kukabiliana na athari za kimbunga Hidaya huko Bagamoyo/ Picha Reuters 

Kimbunga hiki kilisemekana kudhoofika sana kilipokaribia ufukwe wa Tanzania. Hii ilikuwa baada ya umeme kukatika katika sehemu kubwa ya Tanzania Aprili 4, 2024 huku mvua kubwa na upepo mkali utokanao na kimbunga hicho zikinyesha nchini humo kufuatia wiki kadhaa za mafuriko katika eneo hilo.

Vimbunga Afrika

Afrika imekumbwa na vimbunga kadhaa kwa miaka iliyopita ikiwa maeneo ya Afrika Kusini yakiathirika zaidi.

Kati ya Februari na Machi 2023 kimbunga kinachoitwa "Freddy" kiliua watu wasiopungua 1,434. Ikiwa 1,216 waliuawa nchini Malawi, 198 Msumbiji, 17 nchini Madagascar, 2 Zimbabwe, na 1 nchini Mauritius.

Kimbunga Freddy ambacho kilipiga vibaya zaidi nchini Malawi kiligharimu maisha ya watu zaidi ya 1400/ Picha: Reuters

Machi 2022 kulitokea kimbunga kilichoitwa "Gombe" kilichoathiri Msumbiji zaidi. Kimbunga Gombe kiliua watu 63 nchini Msumbiji, 7 Malawi, na 2 nchini Madagascar.

Januari 2021 kimbunga kilichoitwa 'Eloise" kiliuwa watu 27 ikiwa mmoja kutoka Madagascar, 11 Msumbiji, watatu Zimbabwe, 10 Afrika Kusini, na wawili Eswatini.

Aprili 2019 Kimbunga kilichoitwa "Kenneth" kilichoathiri Ushelisheli, Comoros, Mayotte, Madagascar, Msumbiji, Tanzania na Malawi.

Huku, Machi 2019 kimbunga kilichoitwa "IDAI" kiliua watu 1,593 na kuathiri wengine zaidi ya milioni 3 katika nchi za Msumbiji, Malawi, Madagascar na Zimbabwe.

Machi 2019 kimbunga kilichoitwa "IDAI" kiliua watu 1,593 na kuathiri wengine zaidi ya milioni 3 katika nchi za Msumbiji, Malawi, Madagascar na Zimbabwe/ picha: AP

Januari 2018 kimbunga kilichoitwa "AVA" kiliikumba nchi ya Madagascar na kuwaua zaidi ya watu 50.

Kwa nini vimbunga vina majina ya watu?

Mwanzoni vimbunga havikuwa na majina ya watu bali vilipatiwa jina kutokana na mazingira ya kimbunga hicho kinavyotokea.

Tangu mwaka 1953, vimbunga vya kitropiki katika baharí ya Atlantiki vimekuwa vikipatiwa majina kutoka orodha ya Vituo vya Kitaifa vya Kimbunga.

Majina hayo yanahifadhiwa na kuratibiwa na kamati ya kimataifa ya WMO.

Umoja wa Mataifa umeleza kuwa orodha ya awali ilikuwa na majina ya wanawake pekee. Kuanzia mwaka 1979 majina ya wanaume nayo yalianza kujumuishwa.

"Orodha ya wanawake na wanaume hutumika kwa mzunguko ambapo kuna orodha sita. Hii ina maana kwamba orodha ya mwaka 2019 itakuja kurudiwa tena mwaka 2025," UN imesema katika tovuti yake.

TRT Afrika