Jumla ya wagonjwa wawili walikuwa wakipatiwa matibabu hadi kufikia Oktoba 31, 2024./Picha: Menelas Nkeshimana Wizara ya Afya Rwanda

Rwanda imesema imechukua tahadhari ya kuhakikisha hakuna maambukizi mapya ya Marburg ambayo yanasababishwa na popo.

Mnamo Septemba 27, 2024, nchi hiyo ilithibitisha maambukizi ya kwanza wa ugonjwa wa Marburg, unaosababishwa na popo watokao migodini.

" Ukuta umewekwa kwenye mgodi ili kutenganisha eneo la kazi na makazi ya popo. Zaidi ya hayo, timu ya madaktari imetumwa kufuatilia afya ya wafanyakazi kila siku. Hatua kama hizo zimetekelezwa katika migodi mingine ambapo popo hawa wapo," amesema Waziri wa Afya wa nchini Rwanda, Dkt Sabin Nsanzimana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali.

Hadi kufikia Oktoba 31, 2024, jumla ya maambukizi 66 yalikuwa yamethibitishwa, huku wagonjwa 49 wakipona na wengine 15 wakipoteza maisha.

Baada ya kuchunguza asili ya ugonjwa wa virusi vya Marburg nchini humo serikali iligundua kwamba popo wa matunda walihusika na kuenea kwake.

Mgonjwa wa kwanza kugundulika na ugonjwa alikuwa ni mfanyakazi katika moja ya migodi nchini humo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, virusi vya Marburg husalia kwenye maeneo mbalimbali ya miili ya wagonjwa waliopona, kama vile sehemu za ndani za macho, maziwa ya mama na sehemu nyeti, licha ya kutoonekana kwa vipimo vya damu.

" Wagonjwa waliopona bado wanaweza kusambaza virusi kupitia kujamiiana. Hivyo wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuepuka ngono isiyo salama hadi vipimo vithibitishe kuwa virusi vimeondolewa kabisa kwenye mfumo wao," alieleza Dkt Nsanzimana.

Kulingana na Waziri huyo wa Afya wa Rwanda, kuwauwa popo kutaleta changamoto kwani wana jukumu muhimu katika kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na mbu na wadudu wengine na pia ni muhimu katika kilimo.

" Kuna aina nyingi za popo, lakini wale walio na virusi vya Marburg wanajulikana kuishi katika mapango. Popo wanauwezo wa kusambaza virusi mara mbili kwa mwaka, kulingana na msimu wao wa kuzaliana," alieleza Waziri huyo.

Serikali ya Rwanda imeunda timu ya wataalam kuchunguza maeneo mengine ambayo popo hawa wa virusi vya Marburg wanaweza kuwa wanaishi.

Hadi kufikia sasa, Rwanda imepokea dozi 1,700 za chanjo ya Marburg kutoka taasisi ya chanjo ya Sabin iliyoko nchini Marekani.

TRT Afrika