Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Rwanda, FDA, imeziondoa sokoni dawa ya sindano na dawa ya macho, kufuatia malalamiko na wasiwasi wa kiusalama.
Serikali imeamuru kurejeshwa kwa makundi yote ya dawa ya macho ya Tetracycline yaliyotengenezwa na kampuni ya Angel Biogenics Pvt Ltd, India kufuatia malalamiko kuhusu dawa hiyo, FDA ya Rwanda ilisema katika taarifa.
Taarifa hiyo imesema mtengezaji wa dawa ya macho "ameondoa kwa hiari bidhaa hiyo kwa sababu ya kubadilika rangi."
Serikali imeomba wagonjwa walionunua dawa hizo ya macho waache kuitumia.
Mamlaka ya FDA pia imeamuru dawa ya sindano ya Phytomenadione Injection BP 10 mg -1 ml Ampoule ambayo inatengenezwa na kampuni ya Merit Organics iondolewe sokoni.
Mamlaka hiyo imesema dawa hiyo inatofauti ya kiwango cha kemikali au PH, ambayo ni kipimo cha kiwango cha asidi au alkalini.
Waingizaji na wauzaji wa bidhaa hizo mbili wameombwa kuziwasilisha katika mamlaka hiyo ndani ya siku 10, na maelezo kuhusu idadi ya dawa iliyoagizwa, kusambazwa, kurudishwa, na ni wapi ilisambazwa.