Mswada mpya nchini Rwanda unalenga kuboresha maslahi ya kina mama wanaojifungua ilihali bado wanahitajika kurudi kazini.
Pendekezo ambalo iwapo litapitishwa bungeni, kina mama waliojifungua wanaweza kupewa manufaa na malipo ya likizo ya uzazi kwa wiki mbili zaidi kupitia Bodi ya Hifadhi ya Jamii ya Rwanda (RSSB).
Kwa sasa likizo ya uzazi ni wiki kumi na mbili ambayo ni sawa na miezi mitatu.
Hili ni mojawapo ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya Machi 30, 2016 inayosimamia mpango wa mafao ya likizo ya uzazi.
Bima ya faida ya likizo ya uzazi au mpango wa ulinzi wa uzazi ambao huwapa wanawake wanaofanya kazi (kina mama) malipo yao kamili (asilimia 100) wakati wa likizo ya uzazi.
Rasimu ya sheria inapendekeza kwamba RSSB kama msimamizi wa mpango huo, itatoa marupurupu ya likizo ya uzazi yanayolingana na wiki nane za mwisho za likizo badala ya wiki sita zilizotolewa chini ya sheria ya sasa.
Wakati huo huo, mwajiri ataendelea kumlipa mfanyakazi wa kike mshahara kamili katika wiki sita za kwanza. Hii ina maana kwamba, faida ya likizo ya uzazi itatolewa kwa wiki 14 kwa jumla badala ya wiki 12 ya sasa.
Mswada huo pia umezingatia mabadiliko ya likizo ya uzazi yaliyoletwa na sheria ya kazi ya 2023, katika kesi ya uzazi, wakati mama anapoteza mtoto baada ya kuzaliwa.
Kwa mfano, mswada unasema kwamba ikiwa mfanyakazi wa kike atajifungua mtoto njiti, ana haki ya kupata likizo sawa na siku zilizobaki hadi kipindi cha kawaida cha kujifungua cha miezi tisa.
Mwajiri hulipa mshahara wa nusu ya kipindi cha likizo ya uzazi na RSSB inashughulikia nusu nyingine, kulingana na muda uliobaki kabla ya kukamilika kwa miezi tisa ya ujauzito wa kawaida.
Masharti ya mama kupata manufaa ya likizo ya uzazi kupitia bima pia yanatarajiwa kubadilishwa ili kuruhusu mfanyakazi mpya anayejifungua kustahiki malipo ya likizo ya uzazi.
Mswada unatafuta kuondolewa kwa sharti ambalo mama anayefanya kazi lazima awe amechangia mpango wa malipo ya likizo ya uzazi kwa angalau mwezi mmoja kabla ya mwezi wa likizo, ili aweze kustahiki.