Rwanda imekanusha madai ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwamba Kigali inahusika katika kutatiza juhudi za amani mashariki mwa nchi hiyo.
Felix Tshisekedi, Rais wa DRC, alisema katika mahojiano na Radio France Internationale (RFI) na France24 siku ya Ijumaa kwamba makumi ya wanajeshi wa Rwanda hivi karibuni walivuka Mashariki mwa DRC kupigana dhidi ya wanajeshi wa Congo.
Kulingana na Tshisekedi, wanajeshi wa Rwanda "wanajifanya kuwa wanachama wa waasi wa M23."
"Tuna uthibitisho. Kwa silaha tulizonazo, teknolojia tuliyo nayo, tunaziona," Tshisekedi alisema.
Kutuma wanajeshi mpakani 'sio kitu kipya'
Naibu Msemaji wa Serikali ya Rwanda Alain Mukuralinda amekanusha madai hayo na kusema kuwa kutumwa kwa wanajeshi wa Rwanda kwenye mpaka huo sio jambo geni.
"Hata wakati wa amani daima kuna kutumwa kijeshi mpakani. Hakuna mpaka wa taifa lolote duniani unaoweza kuachwa bila ulinzi," Mukuralinda alisema akinukuliwa na gazeti la New Times la Rwanda Jumamosi.
Eneo la Mashariki mwa DRC limekuwa likikumbwa na ghasia kwa miongo kadhaa, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa angalau makundi 100 yenye silaha yanaendesha harakati zake katika eneo hilo lenye hali tete.
Maelfu ya watu wameuawa kwa miaka mingi, na mamilioni ya watu kuyahama makazi yao huku mapigano yakiendelea juu ya udhibiti wa maliasili tajiri, ikiwa ni pamoja na bati na tungsten, katika eneo lenye matatizo.