Mkuu wa wakala wa afya barani Afrika amesema hali katika mji wa Goma nchini DRC imegeukua kwa "dharura ya afya ya umma", akionya kwamba mapigano huko yanaweza kuchochea milipuko ya magonjwa makubwa.
Kundi la waasi la M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limekuwa likisonga mbele katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambalo limekuwa eneo la milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.
Mapema wiki hii, M23 walichukua udhibiti wa sehemu kubwa ya mji mkuu wa Kivu Kaskazini Goma, jiji lenye watu milioni tatu, milioni moja kati yao wakiwa wameyakimbia makazi yao.
Jean Kaseya, mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), alisema ni "hali hizi mbaya, pamoja na ukosefu wa usalama na uhamiaji mkubwa wa watu zimechochea kuenea kwa virusi vya mpox".
Aina ya clade 1b ya mpox, ambayo imerekodiwa katika nchi nyingi ulimwenguni katika miezi ya hivi karibuni, iliibuka kwa mara ya kwanza katika mkoa jirani wa Kivu Kusini mnamo 2023.
"Goma imekuwa kitovu cha maambukizi na kusambaza mpox katika nchi 21 za Afrika," alisema katika barua aliyotuma Ijumaa kwa viongozi wa Afrika.
Hatari ya kuenea magonjwa ya kuambukiza
"Hili si suala la usalama pekee - ni dharura ya afya ya umma," Kaseya alisema.
"Vita hivi lazima vikome. Ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, haitakuwa risasi pekee ambayo itaua maisha - itakuwa ni kuenea kwa milipuko ya ambayo yatatoka katika eneo hili dhaifu na uchumi mbaya wa jamii katika bara letu. ," alisema.
Hali hiyo pia ilisababisha "kuenea kwa surua, kipindupindu na milipuko mingine, ikigharimu maisha ya maelfu zaidi".
Mzozo wa mashariki mwa DRC unaongezeka kwa kasi katika eneo ambalo limeshuhudia miongo kadhaa ya migogoro inayohusisha makundi mengi yenye silaha, ambayo katika miongo mitatu iliyopita yamegharimu maisha ya takriban watu milioni sita.
Waangalizi wa kimataifa wametoa tahadhari juu ya athari za kibinadamu za mzozo unaozidi kuongezeka.