Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) imeahidi kuunga mkono, kulinda uhuru wa kujitawala na uadilifu wa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Ijumaa huku kukiwa na mashambulizi ya kundi la waasi la M23.
Jumuiya hiyo pia ilihimiza kutumwa mara moja kwa mawaziri na wakuu wa ulinzi ili kuhakikisha kuwa ujumbe wa amani wa SADC nchini Kongo (SAMIDRC) unalindwa, wanajeshi wako salama na kuwezesha urejeshaji wa haraka wa wanajeshi waliouawa na waliojeruhiwa.
Zimbabwe ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC Ijumaa huku waasi wa M23 wakidai kudhibiti mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo linapakana na Rwanda.
Pia ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadili mzozo wa mashariki mwa Kongo. EAC ilifanya mkutano tofauti Jumatano na kuitaka Kinshasa kuzungumza moja kwa moja na M23.
Kundi hilo la waasi lilianzisha mashambulizi makubwa wiki iliyopita mjini Goma, mji wenye wakazi takriban milioni 3. Kinshasa imeishutumu Rwanda kwa kutuma wanajeshi kusaidia waasi.
Rwanda imekanusha madai hayo, lakini viongozi wa eneo hilo wametaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, kwani makumi ya watu wamefariki huku mamia wamejeruhiwa.
Uganda pia imeshutumiwa kuwaunga mkono waasi, madai ambayo imekanusha.
Kulingana na ripoti watu 100 wamepoteza maisha yao katika wiki iliyopita, lakini shirika la habari la Anadolu halikuweza kuthibitisha idadi hiyo.
Maelfu wameyakimbia makazi yao, wengi wamekimbilia Rwanda, wakiwemo wafanyakazi kutoka mashirika ya kimataifa kama vile UN na Benki ya Dunia.
Ujumbe wa kulinda amani
SADC imepeleka ujumbe wa kulinda amani mashariki mwa DRC mwezi Desemba 2023.
Nchi ya Afrika Kusini inaongoza kikosi hicho, ambacho kinakadiriwa kuwa na takriban wanajeshi 1,300, wakiwemo wanajeshi wa Malawi na Tanzania.
Taarifa ya mkutano huo ilisema malengo ya ujumbe wa kulinda amani "bado hayajatekelezwa".
Imetaka kutumwa mara moja kwa maafisa wa ulinzi kutoka nchi hizo tatu zenye wanajeshi wa kulinda amani nchini humo ili kuhakikisha wako salama na kuwezesha urejeshaji wa waliouwa na waliojeruhiwa.
"Amani na usalama wa eneo letu ni wajibu wa pamoja," Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, mwenyekiti wa sasa wa SADC, alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo.
"Kwa maana hii, kanda yetu iko tayari kuongeza juhudi za kuwalinda raia wa SADC dhidi ya aina zote za machafuko kulingana na Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa SADC," alisema.
Mkataba huo unasema kwamba shambulio la silaha dhidi ya mwanachama mmoja wa SADC litachukuliwa kuwa tishio kwa amani na usalama wa kikanda na "itakabiliwa na hatua za pamoja kwa haraka".
Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels