Gavana wa zamani na mgombea wa Urais Moise Katumbi. Picha: AFP

Mgombea wa nne amejiondoa katika mbio za uchaguzi ujao wa urais wa DR Congo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu wa Disemba ili kumuunga mkono Gavana wa zamani Moise Katumbi. Hatua ya kujiuzulu kwa Delly Sesanga siku ya Jumapili, inaonekana kama hatua nyengine ya kuimarisha umoja wa upinzani wenye lengo la kutaka kumtoa jasho rais wa sasa Felix Tshisekedi ambae nae anagombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

Kulikuwa na takriban wagombea 26 waliokuwa katika kinyang'anyiro hicho kabla ya kampeni kuanza rasmi mwezi uliopita wa Novemba.

Delly Sesanga, ambae ni mwanasheria na mbunge kutoka jimbo la Kasai-Kati na kiongozi wa chama cha Envol, alitangaza kwamba yeye pia anamuunga mkono Katumbi, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga kusini lenye utajiri wa madini.

"Nimeamua, katika kuimarisha umoja wa kitaifa... ili kuunganisha vikosi vyetu kwa mgombea Moise Katumbi," Sesanga aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kinshasa na katika ujumbe uliowekwa kwenye mitandao ya kijamii.

Awali alimuunga mkono Tshisekedi kwa kura za urais mwaka 2018, lakini tangu wakati huo amekuwa mkosoaji wake mkali, huku akishutumu ahadi zilizovunjwa na "kutokuwa na uwezo wa kunyoosha nchi."

Sesanga alionya kuwa muundo wa duru moja wa uchaguzi uliiweka upinzani katika taifa hilo la Afrika na kuwa na "chaguo dogo, la kutoroka mtego wa kutawanyika kwa kura, ila kuungana."

Wengine waliojiondoa awali na kuchagua kumuunga mkono Katumbi ni pamoja na waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo na wagombea wengine wawili.

AFP