Rais Willim Ruto alivunja baraza la mawaziri 21 kutokana na shinikizo la wananchi wanaotaka mabadiliko ya serikali/ Picha Ikulu Kenya.            

Rais wa Kenya William Ruto hii leo amezungumza na wananchi na kutoa orodha ya kwanza ya majina 11 ambayo yataenda bungeni kukaguliwa kwa nafasi ya baraza la mawaziri.

Kati yao pia ni Mwanasheria Mkuu.

"Ninateua kundi la kwanza la watu 11 kwa ajili ya uteuzi na kuidhinishwa na bunge kwa ajili ya kupitishwa kwa nafasi za makatibu wa baraza la mawaziri na mwanasheria mkuu wa serikali," Rais Ruto amesema katika hotuba kwa taifa.

Hatua hii inakuja baada ya wiki moja tangu Rais avunje baraza la mawaziri 21 kutokana na shinikizo la wananchi wanaotaka mabadiliko ya serikali.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa zamani Kithure Kindiki ameteuliwa na Rais Ruto tena katika nafasi hiyo tena / Picha: Kithure Kindiki

walioteliwa upya

Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa - Kithure Kindiki

Wizara ya Afya - Debra Mulongo Barasa

Wizara ya Ulinzi- Aden Duale

Wizara ya Barabara na Uchukuzi - Davis Chirchir

Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabia nchi na Misitu - Soipan Tuya

Wizara ya Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji - Eric Muga

Wizara ya Elimu- Julius Migosi

Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo- Andrew Muhia Karanja

Wizara ya Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji - Alice Wahome

Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo- Dkt. Andrew Karanja

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali- Dk Margaret Ndungu

Rais amemteua Rebecca Miano kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aden Duale ameteuliwa tena kama katibu wa wizara ya ulinzi / picha: AFP

Majina yajirudia

Katika orodha hiyo mpya, majina sita yaliyokuwa katika baraza lililovunjwa yamejitokeza tena.

Kithure Kindiki, Aden Duale, Alice Wahome , Rebecca Miano, Davis Chirchir na Soipan Tuya.

Maoni ya wananchi

Kutangazwa kwa majina mapya ya mawaziri kumezua mjadala nchini.

Aliyeteuliwa kuwa waziri wa Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji, Alice Wahome tayari ametoa shukrani kwa Rais kupitia akaunti yake ya X.

"Nina heshima kubwa na ninashukuru sana kwa imani mliyoniwekea kwa kuniteua kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri katika Wizara ya Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji," Wahome ameandika.

Wahome ni kati ya walioteuliwa tena baada ya Rais kutengua baraza la awali.

@Wkipchirchir amemjibu " hongera , wewwe ni Mkenya una haki ya kupata fursa ya pili."

"nataka kumpa hongera Rais, amechukua hatua na amesikiza Gen Z, amerudisha waliofaa," Sharon Mohammed, mkaazi wa Eldoret amesema katika mahojiano na vyombo vya habari,

@victorkaleli amesema katika mtandao wa X "Mtu huyu kaunda hawezi kutimiza ahadi zake."

@GenZalerts amesema "Nadhani hilo lilikuwa baraza la mawaziri la Ruto sio la Kenya. Kwa nini uwarudishe baadhi ya watu na sisi tuna mamilioni ya viongozi hapa?"

Rais William Ruto amesema bado anafanya majadiliano zaidi na watu wa sekta mbali mbali ili kupata majina mengine ya makatibu wa baraza.

Katiba inamruhusu rais kuteuwa kati ya mawaziri 14 na 22.

TRT Afrika