Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametimiza miaka 79 wiki hii na katika maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa / Picha: Reuters

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametimiza miaka 79 wiki hii na katika maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa, ameamua kutumia wakati wake kwa kuwasiliana na wananchi wake wa Uganda kupitia mtandao wake.

Rais Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, ni miongoni mwa marais waliokalia kiti hicho kwa muda mrefu zaidi nchini humo. Mara nyingi rais huyo amekuwa akituhumiwa kwa kutawala kwa mabavu.

Hata hivyo, katika barua yake iliyowekwa mtandaoni, ameonyesha kudhihaki tuhuma hizo kwa kusema, ingawa anatuhumiwa kwa udikteta lakini nchi yake ina mfumo wa utawala ambao hata nchi kama Uingereza haina.

“Mfumo wa udikteta unaodaiwa kuwepo nchini Uganda pengine ndio bora zaidi kwani uchaguzi hufanyika mara kwa mara, vikundi ambavyo haviwakilishwi hata nchini Uingereza kama vile wanawake, vijana, walemavu, wazee, wafanyikazi, askari, na kadhalika, wana viti maalum kwenye Bunge na katika halmashauri za wilaya,” imesema sehemu ya barua yake.

Rais Museveni amedai kuwa mwenendo wa mwanasiasa wa upinzani maarufu kama Bobi Wine hauna uwajibikaji/ Picha AP

Kuhusu malalamiko yaliyopo ya upinzani kutopewa fursa za kufanya maandamano na mikutano ya hadhara, rais Museveni amesema suala la nidhamu ndio limechangia.

“Matamasha yameandaliwa, maeneo yamefungwa, watu wanaoingia kwenye kumbi hukaguliwa. Mwenendo wa Bobi Wine hauna uwajibikaji, kama ulivyoongeza maambukizi ya corona kupitia uzembe huo huo. Hivyo ndivyo tulivyopoteza watu 3,291. Kabla ya mikutano hiyo ya kizembe, tulikuwa tumepoteza watu wapatao 300 tu,” aliongeza kusema.

Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine kwa jina lake la usanii, ni mwanasiasa chipukizi nchini humo ambaye anaonekana kuwakilisha sauti ya vijana amewahi kuingia katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2021, nchini humo na kushindwa.

TRT Afrika