Rais Wa Uganda Yoweri Museveni amesema ufisadi nchini humo inaongezeka kwasababu mbinu zlizowekwa kukumbana nayo hazitimizi malengo yake.
" Kwa nini tulitengeneza nafasi za wenyekiti wa mitaa midogo midogo wakati tayari tulikuwa na kamishna wa wilaya, na machifu wa vitongozji ? Sehemu ya tatizo ni kwamba silaha hii ya kupambana na rushwa haitumiki," rais Museveni alisema katika ujumbe aliaandikiwa viongozi wa kidini kwenye mtandao.
"Ikiwa watu waliochaguliwa wamekuwa mafisadi, kwa nini wapiga kura wasiwawajibishe? Viongozi wa kidini wanaweza kupendezwa na hili," aliongezea.
Rais huyo amesema wizi wa ardhi ni mojawapo ya ishara ya ufisadi.
" Unyakuzi wa ardhi ni sehemu ya ufisadi. Unyakuzi wa ardhi haufanyiki mwezini," Rais Museveni amesema.
" Inatokea katika kijiji, parokia, kata ndogo, eneo bunge, wilaya na kadhalika, Kuna miundo ya kiutawala, katika vitengo tofauti vya jamii na kidini. Yote haya yana habari ambayo inaweza kusaidia kwa shida hizi," amesema.
Baba na mwanaye kupambana na ufisadi
Rais Museveni pia amewaambia viongozi wa kidini waangalie suala la uzalishaji mali na ugawaji wa utajiri akida kuwa " kuwa na Watu wasiofanya kazi na kubaki masikini sio kumcha Mungu".
Hata hivyo kiongozi wa chama cha upinani cha NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine , amemkashifu rais Museveni kwa madai kuwa ni yeye ndiye anafanya ufisadi kuendelea.
" Umetekeleza na kuhimiza ufisadi wa kisiasa- kuwahonga wapiga kura na kuwanunua wapinzani wa kisiasa wenye nia dhaifu. Mmenunua ukimya wa viongozi wengi wa kisiasa, kidini na kitamaduni kwa kuwahonga pesa ambazo zinapaswa kuboresha maisha ya watu wetu.," amemjibu rais Museveni mtandaoni.
Wakati huo huo, mwanaye Rais Museveni, Muhoozi Kainerugaba, ameapa kupambana na ufisadi jeshini akiazimia kurejesha usimamizi na uongozi wa kuaminika.
General Muhoozi aliteuliwa na baba yake kama Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.