Rais wa Somalia asaini sheria inayobatilisha mkataba wa bahari wa Ethiopia na Somaliland

Rais wa Somalia asaini sheria inayobatilisha mkataba wa bahari wa Ethiopia na Somaliland

Somalia imetangaza mpango huo kuwa 'haramu,' ikiitisha mkutano wa dharura wa kimataifa.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud asaini sheria akiwa na Maspika wa Bunge la kitaifa na bunge la Seneti. Picha: Ikulu Somalia

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ametia saini sheria inayobatilisha mkataba wa wa bahari uliosainiwa kati ya Ethiopia na eneo la Somalia lililojitenga la Somaliland.

Alitia saini sheria hiyo katika mji mkuu wa Mogadishu, huku Spika wa Seneti ya Somalia Abdi Hashi na Spika wa Bunge la nchi Sheikh Adan Mohamed Nur wakishuhudia.

"Kwa uungwaji mkono wa wabunge wetu na watu wetu, sheria hii ni kielelezo cha kujitolea kwetu kulinda umoja wetu, uhuru na uadilifu wa eneo kulingana na sheria ya kimataifa," Mohamud aliandika kwenye mtandao wa X.

Waziri wa mawasiliano Daud Aweis alisema kuwa sheria hiyo inawakilisha msimamo rasmi wa Somalia na "inafanya kazi kama kizuizi kikubwa dhidi ya uvunjaji wowote katika eneo la Somalia.”

Suldan I. Mohamed, mchambuzi wa kisiasa, aliiambia shirika la habari la Anadolu kuwa sheria hiyo inaashiria jibu kali kutoka kwa wabunge wa Somalia na serikali.

'Kufutilia mbali mpango'

"Somaliland kisheria, chini ya sheria ya kimataifa na kitaifa ni sehemu ya Somalia," alisema. "Sheria inampa Rais Hassan nguvu za kidiplomasia katika hatua ya kimataifa, ikifunga milango juu ya mpango huo.”

Somalia imetangaza mpango huo kuwa 'haramu,' ikiitisha mkutano wa dharura wa kimataifa.

Mkataba huo ulisainiwa mnamo Jumatatu, na kuipa Ethiopia nafasi katika Bahari Nyekundu.

Ethiopia ilipoteza bandari zake za Bahari Nyekundu mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya vita vya Uhuru wa Eritrea, ambavyo viliendelea kutoka 1961 hadi 1991.

Mnamo 1991, Eritrea ilijinyakulia uhuru kutoka Ethiopia, na kusababisha kuanzishwa kwa mataifa mawili tofauti.

Kutenganishwa huko kulifanya Ethiopia ipoteze njia ya moja kwa moja ya kuingia Bahari Nyekundu na bandari muhimu.

Tangu wakati huo, Ethiopia imekuwa bila pwani, ikiathiri uwezo wake wa kufanya biashara ya baharini na bandarini.

AA