Rais wa Kenya Ruto aahidi kukomesha utekaji nyara

Rais wa Kenya Ruto aahidi kukomesha utekaji nyara

Rais William Ruto anawaambia wazazi "kuwajibikia" watoto wao.
Rais wa Kenya Ruto kutoa hotuba ya Hali ya Taifa jijini Nairobi / Picha: Reuters

Rais wa Kenya William Ruto ameahidi kukomesha utekaji nyara, kufuatia visa vya hivi punde vya watu kutoweka ambavyo vimelaaniwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, mawakili na wanasiasa.

Vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki vimeshutumiwa kwa kuwashikilia watu kadhaa kinyume cha sheria tangu maandamano yaliyoongozwa na vijana dhidi ya serikali mwezi Juni na Julai.

Polisi wamekanusha kuhusika lakini wanaharakati wamehoji ni kwa nini wanaonekana kutochunguza kupotea kwa watu hao.

Kutoweka kwa hivi punde kumehusisha hasa vijana ambao wamemkashifu Ruto mtandaoni, huku mashirika ya kutetea haki ya binadamu yakikanusha madai ya polisi kutohusika na kutaka hatua zichukuliwe.

'Wazazi wawajibike'

Akizungumza na umati wa watu Ijumaa huko Homa Bay, mji ulioko magharibi mwa Kenya, Ruto aliahidi kukomesha utekaji nyara huo lakini pia akawaambia wazazi "kuwajibikia" watoto wao.

"Tutakomesha utekaji nyara ili vijana wetu waishi kwa amani," alisema, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

Ruto alikuwa amezungumzia suala hilo katika hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa mnamo Novemba, akikashifu hatua zozote za kupindukia au zisizo za kisheria.

Lakini pia alisema wengi wa kuzuiliwa ni kukamatwa kwa halali dhidi ya "wahalifu na waasi".

Hasira kuongezeka

Hasira imeendelea kuongezeka nchini humo, huku matukio ya hivi punde ya utekaji nyara yakizusha maandamano madogo katika angalau mji mmoja.

"Ikiwa kweli polisi hawajahusika," Chama cha Wanasheria cha Kenya kilisema, lazima "wachunguze na kuwashtaki waliohusika" mara moja.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema mapema mwaka huu kwamba utafiti wake ulielekeza kwenye kitengo kilichotolewa na mashirika mengi ya usalama.

Matamshi ya Ruto yanafuatia maoni ya hivi majuzi ya aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua, ambaye alidai kitengo cha siri ndicho kilihusika na kutoweka kwa watu hao.

TRT Afrika