Polisi wa Kenya wakiwa nchini Haiti kuhakikisha amani inarejea / Picha: Reuters

Huku Marekani ikiwa chini ya uongozi mpya wa Donald Trump, nchi za Afrika zilizokuwa na makubaliano mbalimbali na Marekani wakati wa rais aliyeondoka madarakani Joe Biden zinasubiri kwa hamu kuona iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote.

Kenya ni miongoni mwa nchi hizo, na inategemea kwa kiwango kikubwa udhamini wa Marekani kwa ajili ya ujumbe wake wa usalama nchini Haiti.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi wa Usalama (MSS) uliidhinishwa na Umoja wa Mataifa Oktoba 2023 - zaidi ya miaka miwili baada ya mauaji ya Rais Jovenel Moïse kutokea katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, ambao umekuwa kwa sehemu kubuwa ukidhibitiwa na magenge yenye silaha.

Hadi Kenya sasa imetuma polisi 617 nchini Haiti/ Picha Ikulu Kenya 

Kenya ilijitolea kuongoza vikosi vya amani wakipanga kupeleka maafisa 1000 wa polisi. Hadi sasa polisi waliofika Haiti kutoka Kenya ni 617 huku kukiwa na changamoto kadhaa.Ujumbe huu hauko moja kwa moja chini ya Umoja wa Mataifa, hivyo ufadhili wake hautoki UN, na kutegemea hisani ya nchi zilizoendelea.

Joe Biden alisema Marekani inapanga kutoa zaidi ya dola milioni 300 za usaidizi kwa mpango huo unaoongozwa na Kenya.

Hata hivyo, fedha hizi zote hazijatolewa. Bajeti ya kupeleka vikosi vya usalama nchini Haiti inakadiriwa kuwa takriban dola milioni 600 lakini mpaka sasa, hata nusu ya fedha hizo hazijapatikana.

Maafisa kutoka Guatemala, El Salvador na Kenya Januari 2024 / Picha : Wizara ya Mambo ya Ndani Kenya  

Kufikia Aprili 2024, Canada ilikuwa imetoa Dola milioni 8.7, Ufaransa Dola milioni 3.2 na Marekani Dola milioni 6.

Ujumbe huo pia ulitarajiwa kuwa na idadi ya maafisa 2500, lakini hadi sasa nchi zilizojitolea haijafikisha idadi hiyo.

Mbali na maafisa 617 wa Kenya, maafisa 150 kutoka Guatemala na wengine wachache kutoka El Salvador walifika Haiti mwanzoni mwa mwaka.

Rais Donald Trump huenda akabadilisha sera za kimataifa za nchi yake na haijulikani iwapo ataamua kuendeleza mpango wa kutoa ufadhili au la.

Juhudi za kuendeleza mpango huo uwe chini ya Umoja wa Mataifa hazijafaulu, na haijulikani iwapo Marekani chini ya Donald Trump itaunga mkono wazo hilo au itatumia kura yake ya turufu kupinga mpango huo.

Uwepo wa vikosi vya Kenya nchini Haiti, na amani ya Haiti inategemea kwa kiasi kikubwa uamuzi wa Marekani.

TRT Afrika