Taasisi ya Takwimu ya Rwanda (NISR) imesema kuwa nchi hiyo imepata ongezeko la wawekezaji wa kigeni kulingana na ripoti mpya iliyotoa ya kutathmini uwekezaji.
Takwimu zake zinaonyesha kuwa mitaji ya uwekezaji wa mashirika binafsi ya Kigeni (FPC) nchini Rwanda iliongezeka hadi $886.9 milioni mwaka 2023, kutoka $663 milioni iliyorekodiwa mwaka 2022.
" Hii inachangiwa na kuimarika kwa uchumi," John Rwangombwa , Gavana wa Benki kuu ya Rwanda amesema.
Uwekezaji mkubwa unachangiwa zaidi na mapato kutoka Mauritius, India, Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi. Hii ikiwa ni zaidi ya uwekezaji wa Kenya na China nchini humo.
" Nchi zimewekeza zaidi katika usambazaji wa umeme, gesi, mvuke na viyoyozi na sekta za fedha. India na Kenya zilifuata kwa uwekezaji katika sekta za mawasiliano na Teknolojia, fedha na elimu, wakati ongezeko kubwa liliripotiwa pia kutoka Marekani, Ufaransa na Ujerumani katika mali isiyohamishika, sekta ya viwanda na kilimo," Rwangombwa amesema.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa uwekezaji zaidi ulichangia ajira kwa watu wengi.
Ajira mwaka 2024 ilifikia jumla ya wafanyakazi 59,916. ikijumuisha wazawa 58,415 wakiwa wananchi wa Rwanda na wafanyakazi wa kigeni 1,501 katika nafasi za muda mfupi na muda mrefu.
Hii serikali inasema ilikuwa ongezeko la wafanyakazi 10,126, ikilinganishwa na 49,790 iliyoripotiwa katika mwaka wa 2023.
Gavana wa benki kuu ya Rwanda anasema lengo kubwa la serikali ni kuongeza uwekezaji wa mashirika binafsi mara mbili kutoka dola bilioni 2.2 mwaka 2023 hadi dola bilioni 4.6 ifikapo 2029 kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha uchumi.
Rwanda inatambulika miongoni mwa nchi zenye utaratibu wa kuingia bila viza kwa mataifa ya Afrika na inafahamika kwa kuwa na viwango vya chini vya rushwa pamoja na kuendeleza uwazi katika suala la uchumi," ripoti hiyo imesema kama kichocheo cha kuvutia uwekezaji.