Serikali ya Kenya imeondoa mahitaji ya viza kwa nchi zote za Afrika.
Kenya iilisitisha mahitaji ya viza kwa raia wote wa kigeni kuanzia tarehe 1 Januari 2024, na badala yake kuanzisha mfumo wa Uidhinishaji wa Usafiri wa Kielektroniki (eTA).
Ilikuwa lazima kwa wageni wengi kupata eTA kabla ya kusafiri na iliwagharimu dola 32.50 kama malipo kwa serikali ya Kenya.
Lakini sasa raia barani Afrika hawatohitajika tena kulipa ada hiyo.
" Kama sehemu ya juhudi za kuunga mkono sera za ukuaji wa utalii pendekezo muhimu ni kutoa idhini ya usafiri wa kielektroniki (ETA) kwa nchi zote za Afrika isipokuwa Somalia na Libya kutokana na sababu za kiusalama, " taarifa kutoka kwa kikao cha Baraza la Mawaziri ilisema.
Serikali ya Kenya inasema uamuzi huo unalenga kuimarisha uhusiano na kurahisisha usafiri barani.
" Wageni wengi wataruhusiwa kuwa nchini Kenya kwa miezi miwili huku nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitaendelea kufurahia fursa ya kuwepo nchini kwa miezi sita kulingana na utaratibu wa itifaki ya usafiri ya Jumuiya ya EAC," Mawaziri waliamua.
Kwa nchi zingine zinazohitaji kupata idhini ya usafiri wa kielektroniki (eTA ), serikali imesema itahakikisha kuwa wageni wanaohitaji wanapata majibu ndani ya saa 72.