Africa CDC imethibitisha kuunga mkono juhudi za kuimarisha uwezo wa uchunguzi na vipimo vya maabara nchini Tanzania/ Picha: AFP

Shirika la afya la kudhibiti magonjwa barani, Afrika CDC limesema limeanza kusaidia Tanzania kudhibiti mlipuko ya ugonjwa wa Marburg. Kundi la wataalamu kumi na wawili wa afya ya umma limepelekwa nchini humo katika sehemu zinazoaminika kuwa na maambukizi.

Tanzania imetangaza kuwepo kwa ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) baada ya kuthibitisha maambukizi na kubaini maambukizi mengine 25 yanayoshukiwa kuwa katika Mkoa wa Kagera Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Virusi vya Marburg, ugonjwa unaoambukiza sana na mara nyingi huwa mbaya, ni sawa na Ebola na binadamu hupata maambukizi hayo kutoka kwa popo na nyani.

" Ili kuunga mkono juhudi za serikali, tunatoa dola za Marekani milioni 2 kuimarisha hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa afya ya umma, kuimarisha uchunguzi, na kudhibiti maambukizi," Dkt. Jean Kaseya Mkurugenzi wa Afrika CDC amesema.

Afrika CDC imethibitisha pia kuunga mkono juhudi za kuimarisha uwezo wa uchunguzi na vipimo vya maabara za nchini Tanzania. Vifaa vya kupima tayari vimepelekwa nchini humo pamoja na vifaa vingine vya ziada.

Mwaka 2023 Tanzania ilipata mlipuko wa Marburg, ambao ulisababisha vifo vya watu sita.

TRT Afrika