Nchi za Afrika zimeungana na zingine duniani kutoa pole kwa Uturuki kufuatia ajali ya moto katika hoteli ya Kartalkaya Ski resort, kaskazini mwa Uturuki.
Rais wa Rwanda Paul Kagame alituma salamu zake za rambirambi kwa rais wa Uturuki.
" Rambirambi zangu za dhati kwa Rais Recep Tayyip Erdoğan na watu wa Uturuki kwa vifo vilivyotokana na moto mkali katika kituo cha utalii huko Bolu.Tunawatakia familia za waliofiwa faraja na wote walioathiriwa na msiba huu. Tunawatakia ahueni waliojeruhiwa.”
Moto uliotokea kwenye kituo cha kuteleza kwenye theluji ulisababisha vifo vya takriban watu 76 na kuwajeruhi wengine 51, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya alisema Jumanne.
Kati ya waliojeruhiwa, 17 waliruhusiwa kutoka hospitali huku mmoja akisalia katika chumba cha wagonjwa mahututi, alisema Waziri wa Afya Kemal Memisoglu.
Moto huo ulizuka mwendo wa saa tisa na dakika 27 asubuhi kwa saa za Uturuki katika eneo la mgahawa wa hoteli ya Kartalkaya, na kuteketeza jengo hilo, kulingana na Gavana wa Bolu, Abdulaziz Aydin.
Ethiopia nayo imetoa ujumbe wake kupitia taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje.
" Wizara ya Mambo ya nje Ethiopia inatoa pole kwa familia za waliofiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa ajali hiyo ya moto."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Nigeria pia amewasilisha ujumbe wa serikali yake.
" Serikali ya Nigeria inatoa rambirambi kwa serikali ya Uturuki na familia za walioathirika na ajali hiyo ya moto, na pia inawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa." Kimiebi Ebienfa amesema katika taarifa.
Siku ya taifa ya maombolezo
Uturuki imetangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa siku ya Jumatano.
Rais Recep Tayyip Erdogan Jumanne alitoa salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao, na kuwaombea faraja na kupona haraka kwa waliojeruhiwa.
Aliwahakikishia wananchi kuwa waliohusika na maafa hayo, iwe kwa uzembe au utovu wa nidhamu, watawajibishwa.