Rais Samia alimtaja Dr Salim kama kinara wa diplomasia aliyeimarisha mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine/ Picha : Ikulu Tanzania

Na Idd Uwesu

TRT Afrika, Dar Es Salaam, Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi tovuti ya hifadhi ya Nyaraka za aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi huru za Afrika OAU na Waziri Mkuu wa Tanzania Dr Salim Ahmed Salim

Katika hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dar es salaam katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Samia amesema Afrika inajivunia uongozi wa Dr Salim na kwamba uzoefu wake sasa utaweza kuwanufaisha wengi huku ukitoa somo kwa viongozi wengine juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu za kazi zao.

“Dr Salim Ahmed Salim alijipanga mapema kutaka kuweka kumbukumbu za maisha yake, na naweza kufikiria kuwa pengine hata alikusudia kuandika kitabu chake. Lakini badala yake kwa kuwa amekuza vijana mahiri akina Ahmed na wenziwe, kitabu kile kimewekwa kwa njia ya kidijitali kwa kutumika teknolojia ya kisasa” allisema Rais Samia

Aidha Rais Samia alimtaja Dr Salim kama kinara wa diplomasia na kuongeza kuwa Wakati akiwa katika utumishi wake aliboresha mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine na kusababisha matokeo chanya katika uchumi wa Tanzania

“Mahusiano haya mazuri baina ya China na Tanzania yalisaidia uanzishwaji wa viwanda mbalimbali kikiwemo kiwanda cha nguo za urafiki, na baadaye reli ya TAZARA hapa nchini”

Rais Samia Suluhu Hassan

Balozi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuteuliwa

katika kuenzi mchango wa Dr Salim Ahmed Salim, Rais Samia alitangaza kuwa chuo cha diplomasia kilichopo jijini Dar es salaam sasa kitaitwa jina la Dr Salim na kwamba rasmi kitajulikana kama ‘Dr. Salim Ahmed Salim Center for Foreign Relations’

Dkt Salim Ahmed Salim amesifiwa kama kiongozi aliyewapa wengi walio chini yake furs aya kukua / Picha : Ikulu Tanzania

Baadhi ya viongozi waliopata kufanya kazi na Dr Salim Ahmed Salim akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amemuelezea Kiongozi huyo mwenye historia ya kuteuliwa kuwa Balozi akiwa na umri wa miaka 22 kama kiongozi mwenye uwezo mkubwa.

“Salim alipokua Waziri Mkuu aliwashangaza wengi. Anajifunza mengi sana tena kwa muda mfupi. Alizunguka nchi hii akaelewa matatizo na alikuwa akienda mahali popote akakuta kuna tatizo ambalo ni la utendaji na halihitaji sera akitoka huko anakuja anatoa maelekezo nini kifanywe” alisema Jaji Warioba.

Balozi Amina Ally katika maelezo yake kuhusu Dr Salim amemueleza kama Kiongozi Mlezi ambae alipenda kuwapa nafasi watu wa chini kujifunza na kukua katika majukumu yao.

“Wakati nakwenda Umoja wa Afrika, aliniita Dar es salaam akaniambia kuna nafasi zinatakiwa wanawake waende kule Umoja wa Afrika, mimi nikamwambia Muheshimiwa nimefanya kazi wizara ya mambo ya nje kama Waziri lakini mengine sina uzoefu nayo, akasema hapana nakuamini na utaweza, nenda. Baadae nikaenda na bado akawa kimbilio langu kila Wakati namuuliza” alisema Balozi Ally.

Kwa mujibu wa msemaje wa familia ambaye ni mwanaye Ahmed Salim, kazi ya kuunda tovuti hii ilianza Oktoba 2021 ikijumuisha :

  • Picha zaidi ya elfu kumi na mbili za matukio mbalimbali ya Dr Salim.

  • Machapisho ya nakala za magazeti na majarida yenye taarifa kumuhusu.

  • Dondoo alizokua akiandika yeye mwenyewe Dr Salim kuhusu matukio mbalimbali katika kipindi chote cha utumishi wake.

Rais Samia amesema Afrika inajivunia uongozi wa Dr Salim na kwamba uzoefu wake sasa utaweza kuwanufaisha wengi / Picha : Ikulu Tanzania 

Tumaini letu ni kuwa makumbusho haya ya kidijitali yatatunza historia njema na adhimu ya Tanzania katika Bara la Afrika na kutoa hamasa kwa viongozi na watumishi wa umma katika kutafuta diplomasia ya uchumi kwa ajili ya taifa letu linaoendelea kukua” alisema Ahmed Salim.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa akiwemo Rais Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete pamoja na wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa.

TRT Afrika