Serikali ya sasa kama ilivyokuwa katika serikali zingine zote zilizotangulia Kenya, zinakumbwa na tatizo la maskwota katika misitu na hifadhi za serikali. / Picha : X - William Ruto 

Rais wa Kenya William Ruto amewaagiza maskwota wote waliokita kambi katika misitu iliyohifadhiwa kuondoka mara moja kabla ya kukabiliwa na sheria.

Rais Ruto alitoa agizo hilo alipohutubia ibada ya mazishi mjini Narok takriban kilomita 140 nje ya Nairobi.

''Tunawataka wote waliovamia misitu yetu, hasa msitu wa Mau, waondoke na hiyo sio ombi,'' alisema Rais Ruto.

Ruto pia amesema kuwa wanafanya juhudi kuzungushia uzio misitu muhimu yenye chemicheni ya maji.

"Tutaweka uzio kuzunguka minara yote ya maji nchini ili kuilinda dhidi ya kuvamiwa. Hii ndiyo sababu ninawaomba wale ambao wamevamia kuhama mara moja,” akaongeza Rais Ruto.

Msitu wa Mau ni muhimu zaidi kati y amisitu mingine kumi inayotazamiwa kama vyanzo vikuu vya maji asili ya Kenya.

Hata hivyo kumekuwa na vuta nikuvute kwa miaka mingi kutokana na maskwota waliovamia msitu huo ambao wanalaumiwa kuharibu vyanzo vya maji na kukata miti kwa ajili ya matumiz iya ardhi hiyo.

Kufurushwa kwa maskwota kutoka eneo la vyanzo vya maji kulianza mwaka wa 2005 chini ya utawala wa Rais wa zamani Mwai Kibaki, wakati serikali ilipobatilisha hati miliki zote katika eneo la Mau.

Msitu wa Mau ni kati ya maeneo kubwa zaidi ya vyanzo vya maji katika eneo la Afrika Mashariki linalofunika ekari 675,000 katika Bonde la Ufa.

Kwa sasa Msitu wa Mau unasimamiwa na shirika la misitu nchini Kenya, KFS.

Hatua kama hii ya kuwafukuza maskwota kutoka misitu na ardhi za hifadhi, imekumbwa na pingamizi katika takriban kila serikali, na wengi wanaamini kuwa kwa kiasi kikubwa inachochewa na wanasiasa.

TRT Afrika